Mkurugenzi wa mashindano ya NIACHEKONA CUP 2026, Paul
Daud Augustino maarufu MC NIACHEKONA, amewashukuru Watanzania, wadau wa
michezo, washiriki na taasisi mbalimbali zilizochangia kufanikisha mashindano
hayo yaliyomalizika salama baada ya zaidi ya mwezi mmoja wa ushindani.
Akizungumza mara baada ya fainali kumalizika katika
Uwanja wa Mwabenda, Kata ya Solwa, Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, MC
NIACHEKONA amesema mashindano hayo yalianza rasmi Mei 16, 2026 yakishirikisha
jumla ya timu 22 kutoka maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Shinyanga na mikoa jirani.
Amesema kati ya timu hizo, Kashishi FC kutoka Kata ya
Solwa imefanikiwa kutwaa ubingwa wa mashindano hayo huku Ufukunyungu FC kutoka
Mjini Shinyanga ikimaliza katika nafasi ya pili baada ya kufika fainali.
MC NIACHEKONA ametoa shukrani za dhati kwa wananchi na
wadau wote waliojitokeza kuunga mkono mashindano hayo tangu mwanzo hadi mwisho.
"Nawashukuru Watanzania wote kwa
kuweza kutusapoti. Nawashukuru Misalaba Media, Jambo FM, Lushu Foundation
pamoja na wadau wengine wote tuliokuwa tukishirikiana nao katika kufanikisha
mashindano haya," amesema.
Aidha, ametoa pongezi kwa Kamati ya Mashindano,
waamuzi, watangazaji wa michezo na watu wote waliohusika katika usimamizi wa
michuano hiyo, akisema mchango wao umewezesha mashindano hayo kumalizika kwa
mafanikio makubwa na amani.
MC NIACHEKONA pia ameomba serikali kuendelea kuunga
mkono juhudi za kuendeleza michezo ya vijana, akieleza kuwa mwitikio mkubwa wa
wananchi na washiriki unaonesha umuhimu wa michezo katika jamii.
Amesema anaamini kupitia Ofisi ya Afisa Michezo wa
Wilaya pamoja na mamlaka husika, ujumbe wake utafikishwa serikalini ili
kuendelea kuweka mazingira mazuri ya maendeleo ya michezo na vipaji vya vijana.
Aidha, ameshukuru Serikali, Chama cha Mpira wa Miguu
pamoja na taasisi mbalimbali za michezo ikiwemo SHIDEFA kwa ushirikiano na
vibali vilivyowezesha mashindano hayo kufanyika kwa mujibu wa taratibu na
sheria.
Mashindano ya NIACHEKONA CUP 2026 yalihusisha timu 22
ambazo ni Home Boys, Manheigana, Ufukunyungu FC, Mwasenge, Duara FC, Mwandutu,
Shilima, Songambele Mhangu FC, Nyundo FC, Nzoza, Mahembe, Mawemiru FC,
Nyandolwa FC, Bajaji FC, Shilabela FC, Lyabukande, Kimandaguli, Kashishi FC,
Isenengeja, Mwakitolyo No. 6, Sangu FC na Bulige FC.
Mashindano hayo yameandaliwa na Paul Daud Augustino
maarufu MC NIACHEKONA kwa ufadhili wa Lushu Foundation, yakilenga kuibua vipaji
vya vijana, kukuza michezo na kuimarisha mshikamano wa jamii.
KASHISHI FC YAANDIKA HISTORIA KWA KUTWAA UBINGWA WA NIACHEKONA CUP 2026
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254

Post a Comment