Na Mwandishi Wetu
Uwekezaji mkubwa unaofanywa na serikali katika kupanua elimu ya ufundi stadi nchini unatajwa kuwa mwarobaini utakaomaliza kabisa changamoto ya ukosefu wa ajira kwa vijana na kuwazika katika shughuli za uzalishaji mali, kupitia ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya vyuo vya VETA.
Hatua hii itawawezesha vijana wengi kote nchini kupata ujuzi wa vitendo utakaowaondoa vijiweni na kuwapa fursa ya kujiajiri au kuajiriwa kwa urahisi.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wanu Hafidhi Ameir, aliliambia bunge kuwa mkakati huo unatekelezwa kupitia Mradi wa Pili wa Elimu na Ujuzi kwa Ajira Zenye Tija (ESPJ II), unaolenga kuwabadilisha vijana kuwa nguvu kazi yenye tija na yenye shughuli za kufanya muda wote.
Katika kuhakikisha vijana maeneo ya vijijini wanajazwa ujuzi na kuwa 'bize' na kazi, serikali imetenga shilingi bilioni 1.8 kwa ajili ya kukarabati Chuo cha VETA Ulyankulu mkoani Tabora.
Akijibu swali la Mbunge wa Ulyankulu, Japhael Lufungija, Naibu Waziri Wanu alieleza kuwa kazi za awali zikiwemo za majengo ya utawala na karakana zimeshakamilika kwa asilimia 93.5, hatua itakayofungua milango kwa vijana wengi wa eneo hilo kupata ujuzi utakaowaingiza moja kwa moja kwenye sekta ya uzalishaji na kuachana na utepetevu.
Wakati huo huo, mkakati huo unaenda sambamba na ukamilishaji wa Chuo cha VETA Wilaya ya Kigamboni mwezi Agosti 2026, ambacho kitakuwa kimbilio la vijana wa Dar es Salaam wanaosaka ujuzi utakaowaondoa kwenye utegemezi.
Akijibu swali la Mbunge wa Kigamboni, Faustine Ndugulile (aliyetajwa kama Haran Sanga bungeni), Wanu alisema serikali imetenga shilingi bilioni 2.34 kwa ajili ya vifaa vya mafunzo nchi nzima, ambapo shilingi milioni 36 zitaenda Kigamboni ili vijana wakute kila kitu tayari, jambo litakalowapa motisha ya kujikita kwenye masomo ya ufundi na hatimaye kuanzisha karakana na biashara zao.
Ujenzi huu wa Kigamboni ni sehemu ya mpango kabambe wa serikali wa kujenga vyuo 65 vya VETA katika wilaya 64 pamoja na Mkoa wa Songwe, maeneo ambayo hapo awali yalikuwa hayana fursa hizo.
Kusogezwa huku kwa vyuo vya ufundi katika ngazi ya wilaya kunatarajiwa kubadilisha kabisa mtindo wa maisha ya vijana nchini, kwani kutawapa mazingira ya kujifunza kazi za mikono, kuwatoa kwenye wimbi la uhalifu na unyanyasaji, na badala yake kuwapa maisha mapya yenye misingi imara ya kiuchumi kupitia ajira za uhakika.
SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254
Post a Comment