Na Seif Mangwangi, Arusha
WANAFUNZI wanaofanya ubunifu wa matumizi ya teknolojia mbalimbali katika chuo cha ufundi Arusha (ATC), wamegundua teknolojia mpya ya kupiga kura kidigitali ukiwa nyumbani bila ya kufika kwenye kituo cha kupigia kura.
Akizungumza wakati wa kilele cha kufunga maonyesho ya tatu ya ubunifu chuoni hapo, Juni 19, 2026 Mkuu wa chuo hicho Profesa Mussa Chacha amesema bunifu zinazofanywa na wanafunzi chuoni hapo ni faida Kwa maendeleo ya watanzania.
Amewataka wanafunzi hao kusoma Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kuielewa na kuona fursa zilizopo ndani yake na kufanya bunifu zao kutokana na malengo ya dira hiyo.
Profesa Chacha amesema dira ya Taifa 2050 imeainisha maeneo ambayo yanapaswa kuendelezwa kwaajili ya Maendeleo ya Watanzania hivyo wanafunzi wanaofanya bunifu chuoni hapo wanapaswa kuyasoma na kuyajua na kuyafanyia ubunifu.
Amesema kutokana na kazi nzuri ya ubunifu ambayo imekuwa ikifanywa na wanafunzi chuoni hapo, chuo kimepanga kujenga jengo maalum la ghorofa nne ambalo litatumika kwaajili ya shughuli za ubunifu.
“ Kwa kushirikiana na Serikali ya Italia hivi karibuni tunatarajia kujenga jengo kubwa la ghorofa nne ambalo litatumika kwaajili ya shughuli za ubunifu( innovation), hapa chuoni hatutaki hivi vipaji vyenu vipotee,” amesema.
Aidha Profesa Chacha amesema chuo kinaendelea na ujenzi wa karakana ( industrial workshop), ambayo itatumika kutengeneza mitambo bunifu itakayokuwa ikigunduliwa na wanafunzi chuoni hapo kwaajili ya kuuzwa na kwamba tayari mashine zitakazotumika katika karakana hiyo zipo njiani kufika chuoni hapo.
“ Hivi sasa tumeamua kuendeleza bunifu zote zitakazobuniwa na wanafunzi Kwa kuzizalisha na kuziingiza sokoni, tutakuwa na kiwanda hapa hapa chuoni na wote mnaofanya ugunduzi huu tutaendelea kuwafuatilia na kuona namna mnafaidika na bunifu zenu, tutawashika mkono popote mtakapoenda,” amesema Profesa Chacha.
Aidha amesema chuo kinakamilisha jengo la hospitali itakayokuwa ikitibia wanafunzi chuoni hapo lakini pia chuo kipi kwenye mikakati ya kujenga jengo litakalojulikana kama innovation center ambalo litakuwa maalum kwaajili ya ugunduzi na uzalishaji wa vifaa tiba vya hospitalini ( biomedical engineering).
Awali akimkaribisha mgeni rasmi Makamu mkuu wa chuo, Dkt Yusuph Mhando alisema katika maonyesho ya mwaka huu ambayo ni awamu ya tatu tangu kuanzishwa, jumla ya bunifu 75 ziliingia kwenye ushindani.
Amesema kati ya bunifu hizo, bunifu 20 zilihusiana na teknolojia ya habari na mawasiliano(Tehama), umeme 15, mitambo na magari 19, sayansi timizi 8, ujenzi na barabara13 na kwamba baada ya majaji kupitia bunifu hizo jumla ya bunifu 19 pekee ziliweza kuingia fainali.
Amesema mshindi wa kwanza ametoka katika fani ya mitambo aliyegundua mashine inayojulikana kama ( Energy trauma kit), akifuatiwa na Tehama ambaye amegundua mashine ya kupima uoni wa macho ( VR acute test),
Aidha amesema maonyesho hayo ni muhimu Kwa Taifa Kwa kuwa yamekuwa yakikuza ujuzi wa wanafunzi chuoni hapo Kwa kuweza kuonyesha Kwa vitendo kile ambacho wamekuwa wakifundishwa darasani.
“ Katika bunifu hizi, Kuna vijana wametengeneza mfumo wa kupiga kura wakati wa uchaguzi ukiwa nyumbani, teknolojia hii ikiweza kuboresha itaweza kusaidia sana katika eneo hili,” amesema.
Amesema ni tegemeo la chuo kuwa bunifu hizo zitafikia jamii na kutatua kero mbalimbali inazizikabili na hivyo chuo kitaendelea kuimarisha na kuendeleza vipi vya wanafunzi hao.









Post a Comment