
NA DENIS MLOWE, IRINGA
BARAZA la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Iringa limesisitiza umuhimu wa halmashauri kuendelea kulipa madeni ya watumishi na wazabuni sambamba na kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani ili kuongeza uwezo wa kutekeleza wajibu huo kwa wakati.
Msisitizo huo umetolewa katika kikao cha Baraza la Madiwani baada ya mjjumbe kujadili taarifa ya kamati ya fedha.mipango na utawala
na kueleza wasiwasi wao kuhusu ongezeko la madeni ya watumishi na wazabuni.
Akichangia mjadala huo, Diwani wa Kata ya Lumuli, Abeid Kisinini, alisema halmashauri inapaswa kuwa na mkakati wa kuhakikisha madeni hayo yanapungua kwa kuwa yanawaathiri watumishi na wazabuni waliotekeleza majukumu yao kwa mujibu wa mikataba.
Alisema taarifa ya utekelezaji wa bajeti inaonyesha watumishi wanadai takribani Sh bilioni 1.7 huku kiasi kilicholipwa katika mwaka wa fedha 2025/2026 kikiwa Sh milioni 231.2 pekee. Aidha, alisema wazabuni wanadai zaidi ya Sh bilioni 1.7 wakati malipo yaliyofanyika ni Sh milioni 34.5.
Akijibu hoja hizo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, Robert Masunya, alisema sehemu ya madeni ya watumishi imetokana na uhamisho wa watumishi kutoka Manispaa ya Iringa kwenda Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, huku madeni ya wazabuni yakichangiwa na upungufu wa mapato ya ndani ukilinganishwa na makadirio ya bajeti.
Alisema halmashauri imetenga Sh milioni 362.3 katika mwaka wa fedha 2026/2027 kwa ajili ya kulipa madeni hayo, zikiwemo Sh milioni 317.2 za wazabuni na Sh milioni 45.1 za watumishi.
Masunya alisema uwezo wa kulipa madeni utaongezeka endapo ukusanyaji wa mapato ya ndani utaimarishwa na kufikia malengo yaliyowekwa.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, Steven Mhapa, aliwataka madiwani, watendaji na wananchi kushirikiana kuongeza ukusanyaji wa mapato ili halmashauri iwe na uwezo mkubwa wa kulipa madeni pamoja na kuendelea kutekeleza miradi ya maendeleo.
Alisema hakuna halmashauri inayopenda kuwa na madeni, hivyo kila mmoja anapaswa kutimiza wajibu wake katika kuongeza mapato yatakayowezesha kuboresha huduma na kulipa wadai kwa wakati.
Naye Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Iringa Vijijini, Costantino Kihwele aliyepewa nafasi kama mgeni mwalikwa alisema ukusanyaji wa mapato ni msingi wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo na ulipaji wa madeni, akiwataka wananchi kuendelea kutimiza wajibu wao wa kulipa kodi, ushuru na tozo mbalimbali kwa mujibu wa sheria.
Alisema ushirikiano kati ya wananchi, madiwani na watendaji utaisaidia halmashauri kuongeza mapato na kuimarisha utoaji wa huduma pamoja na kupunguza mzigo wa madeni ya watumishi na wazabuni
Post a Comment