
Na Eleuteri Mangi, Dodoma
Tanzania inaendelea kufanya mageuzi makubwa katika sekta ya ardhi kwa kuimarisha mifumo ya kidijiti na matumizi ya teknolojia za kisasa za taarifa za kijiografia ili kuimarisha usimamizi wa Sekta ya Ardhi nchini.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Leonard Akwilapo alipofanya mazungumzo na Balozi wa Korea nchini Tanzania Mhe. Eunju Ahn, jijini Dodoma Julai 15, 2026 na kusisitiza kuwa uhusiano uliopo baina ya nchi hizo mbili ni daraja la kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia, kiuchumi na kiteknolojia kati ya Tanzania na Jamhuri ya Korea katika sekta ya ardhi.
“Katika safari hii ya mageuzi, ushirikiano wetu na Jamhuri ya Korea pamoja na Kituo cha Taifa cha Ubunifu na Taarifa za Kjiografia (TNGC) ni nguzo muhimu inayochangia kufanikisha dira ya Serikali ya kujenga sekta ya ardhi, yenye ufanisi na inayotumia teknolojia za kisasa” alisema Dkt. Akwilapo.
Aidha, Tanzania imepata mafanikio makubwa katika kujenga uwezo wa wataalamu wa Kitanzania kupitia mafunzo ya mifumo ya taarifa za kijiografia (GIS), utengenezaji wa ramani kwa kutumia ndege zisizo na rubani, upimaji kwa kutumia teknolojia za satelaiti pamoja na usimamizi wa ardhi kwa njia za kidijiti ili kujenga kizazi cha wataalamu wenye uwezo wa kuongoza maendeleo ya sekta ya taarifa za kijiografia na kuchangia uchumi wa kidijitali nchini
Jitihada hizo zinachangia Serikali kuboresha usajili wa ardhi, kuimarisha Miundombinu ya Kitaifa ya Takwimu za Kijiografia (NSDI), kuongeza usalama wa umiliki wa ardhi, kupunguza migogoro ya ardhi na kuwezesha maendeleo jumuishi na endelevu kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.
Kwa upande wake Balozi wa Korea nchi Mhe. Eunju Ahn amesema Korea inatambua umuhimu wa Tanzania kuimarisha mifumo ya kielekroniki katika sekta ya ardhi kwa kuzingatia Dira 2050 na ni kipengele muhimu kwa maendeleo ya taifa.
Balozi Mhe. Eunju amesisitiza kuwa vifaa vilivyopo katika Kituo cha Taifa cha Ubunifu na Taarifa za Kjiografia (TNGC) vitunzwe ili viendelee kuleta tija kwa kuwafundisha watumiaji wengi zaidi katika sekta ya ardhi.
Awali Mkuu wa Kituo cha Taifa cha Ubunifu na Taarifa za Kjiografia (TNGC) Dkt. Aidan Kawinga amesema hadi sasa kituo hicho kimetoa Wakufunzi 19 na wataalam 63 katika mafunzo ya Mifumo ya Taarifa za Kijiografia (GIS), Urubani wa Ndege Nyuki na Upimaji Ardhi kwa kutumia satelaiti.

Post a Comment