" SERIKALI YASISITIZA UMAKINI KULINDA AMANI, YATAKA WANANCHI NA VIONGOZI WA DINI KUSHIRIKIANA

SERIKALI YASISITIZA UMAKINI KULINDA AMANI, YATAKA WANANCHI NA VIONGOZI WA DINI KUSHIRIKIANA

 



SERIKALI imesema ipo makini kuhakikisha nchi inaendelea kuwa na amani, huku ikitoa wito kwa wananchi na viongozi wa dini kutochukua amani hiyo kimzaha.
Hayo yalisemwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi, wakati akimwakilisha Makamu wa Rais, Dk Emmanuel Nchimbi, katika maadhimisho ya miaka 40 tangu kuzaliwa kwa Kanisa la Elim Pentekoste wilayani Karatu Mkoa wa Arusha, maadhimisho yaliyokwenda sambamba na kutimiza miaka 40 ya uongozi wa Askofu Mkuu wa kanisa hilo, Peter Konki. Katika hafla hiyo, Waziri Katambi alikabidhi Sh milioni 10 kutoka kwa Makamu wa Rais ikiwa ni mchango wa ujenzi wa kupaua kanisa hilo.

Akizungumza kwenye maadhimisho hayo, Waziri Katambi alionya kuwa taifa linawindwa kutokana na rasilimali zake na kwamba vita na migogoro mingi duniani leo inasababishwa na tamaa ya mali na madaraka, hali inayowaathiri zaidi wananchi wa kawaida wakiwemo akina mama, watoto, wazee na wenye ulemavu ambao hawawezi kujihami.

Alisisitiza kuwa Tanzania ina historia nzuri ya amani na ya kuwalea wakimbizi kutoka nchi zenye machafuko, hivyo ni wajibu wa kila mmoja kujifunza kutokana na makosa ya nchi nyingine badala ya kusubiri kufanya makosa wenyewe ndipo wajifunze.

Waziri Katambi aliwaomba viongozi wa dini waisaidie serikali kuwaelewesha wananchi kuhusu umuhimu wa amani, akibainisha kuwa ingawa makundi yote katika jamii yana haki sawa kikatiba, changamoto hutokea pale kundi moja linapotaka kuchukua haki za wengine. Aliwakumbusha wananchi kuwa endapo nchi itapata machafuko, hakuna sehemu salama ya kukimbilia, na kuwataka kuendelea kulinda mshikamano uliopo.

Kwa upande wake, Askofu Konki alihakikisha kuwa kanisa litabaki kuwa sehemu ya amani ya Tanzania na kusisitiza kuwa masuala ya maridhiano ni ya msingi huku akiongeza kuwa upendo ndiyo karama kuu inayopaswa kuongoza jamii kwa kuwa unasamehe na kuchukuliana. Askofu Konki aliwakumbusha wananchi kuwa nchi haijengwi kwa kulalamika kila siku, bali kupitia kuwasilisha hoja kwa viongozi na kusubiri majawabu yao.

Post a Comment

Previous Post Next Post