
Innocent Mungy
Wadau wa mawasiliano wamesema kuwa wanaotumia vibaya mitandao kwa kusema uongo au kudhalilisha wanapaswa kutambua adhabu kali zinazowakabili, wakitolea mfano uamuzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Accra nchini Ghana iliyomhukumu mshawishi maarufu katika mtandao wa TikTok, Camilla Alhassan kifungo cha mwaka mmoja gerezani baada ya kukiri makosa ya kusambaza taarifa za uongo na kufanya tabia ya kuudhi dhidi ya Rais John Dramani Mahama.
Akizungumzia tukio hilo, mtaalamu wa mawasiliano, Innocent Mungy amesema kuwa hapa nchini mtu anayechapisha taarifa za uongo, kumsingizia mtu au kumtukana mtandaoni anaweza akafungwa au kutozwa faini, huku akisisitiza kuwa hakuna mtu mwenye mamlaka ya kumsemea mwingine kinyume cha sheria.
Aliongeza kuwa kitendo cha kuweka mtandaoni taarifa binafsi za uongo kinakiuka sheria za ulinzi wa taarifa binafsi na usalama wa mtandao, ambazo zimetungwa kama sheria pacha za kuzuia udhalilishaji, huku akibainisha kuwa hata upande wa dini kusema uongo na kuchafua wengine ni dhambi, na ujumbe kutoka Ghana ni kuwa watu wanapaswa kutumia mawasiliano kwa weledi na umakini mkubwa.
Kwa mujibu wa Sheria ya Makosa ya Mtandao ya Mwaka 2015, utoaji wa taarifa za uongo au unyanyasaji mtandaoni una adhabu ya faini isiyopungua Sh milioni tano au kifungo kisichopungua miaka mitatu, au vyote kwa pamoja, wakati udanganyifu unaohusiana na kompyuta una adhabu ya faini isiyopungua Sh milioni 20, au mara tatu ya thamani ya faida iliyopatikana kinyume cha sheria, au kifungo kisichopungua miaka saba, au vyote kwa pamoja.
Naye mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Dk Mary Kafyome, alisisitiza kuwa kila mtu ana haki ya kutoa maoni lakini sharti itumike kwa uwajibikaji, akionya kuwa mitandao si mahali pa kusambaza uongo au matusi, na kuwataka wananchi kujitathmini kwa kujiuliza ukweli, manufaa na staha ya taarifa kabla ya kuzisambaza.
Aliongeza kuwa kukosoa kunaruhusiwa katika jamii ya kidemokrasia mradi kuwe na hoja na heshima, na akasisitiza kuwa familia, shule, vyuo, taasisi za dini na vyombo vya habari vina wajibu wa kukuza maadili ya teknolojia wakati vyombo vya sheria vikiendelea kutoa elimu na kusimamia sheria kwa haki na uwazi.
Kwa upande wake, mtaalamu wa mawasiliano na mchambuzi wa masuala ya kijamii, Faida Katea, alisema kuwa nchi inatakiwa kuendelea kusimamia sheria kikamilifu kwa kutoa adhabu kwa wanaokiuka misingi hiyo, akitolea mfano Ghana kuwa na msimamo mkali kwenye masuala ya sheria za mitandao uliowezesha kuchukua hatua stahiki.
SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254
Post a Comment