" SERIKALI YAZINDUA MRADI WA MIKOPO NAFUU UJENZI WA VITUO VIDOGO VYA MAFUTA VIJIJINI

SERIKALI YAZINDUA MRADI WA MIKOPO NAFUU UJENZI WA VITUO VIDOGO VYA MAFUTA VIJIJINI

 

📌 Mradi unatekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kupitia Benki ya AZANIA

📌 Lengo la Mradi ni kupunguza kwa kiwango kikubwa biashara hatarishi ya kuuza mafuta kwenye chupa za plastiki na vyombo visivyokidhi viwango vya usalama

📌 Wanufaika nane (8) watengewa kiasi cha shilingi bilioni 1

Dar es Salaam📍

Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa ushirikiano na Benki ya Azania imezindua rasmi mradi mkubwa wa utoaji wa mikopo nafuu kwa wajasiriamali wadogo, utakaofanikisha ujenzi na uendeshaji wa vituo vidogo vya kuuza mafuta ya petroli na dizeli maeneo ya vijijini.

Hatua hiyo inalenga kuongeza upatikanaji wa nishati ya mafuta, kupunguza gharama zisizo za lazima kwa wananchi na kuchochea ukuaji wa uchumi katika maeneo hayo.

Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya utiaji saini wa mikataba kwa wanufaika nane wa kwanza, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati (Mafuta na Gesi), Dkt. James Mataragio, alisema serikali imeamua kusogeza huduma hiyo karibu na wananchi ili kumaliza changamoto ya kutembea umbali mrefu kufuata nishati hiyo.

"Mafuta ni nguzo muhimu ya maendeleo ya uchumi na ustawi wa jamii. Mpango huu utasaidia kupunguza tofauti kubwa ya bei kati ya mijini na vijijini, ambapo awali maeneo mengine wananchi walilazimika kununua mafuta kwa bei inayozidi mara mbili ya ile ya mijini," alisema Dkt. Mataragio.

Dkt. Mataragio aliongeza kuwa ujenzi wa vituo rasmi utaondoa hatari za moto na ajali zinazotokana na uuzaji au uhifadhi wa mafuta kwenye chupa za plastiki na magaloni yasiyokidhi viwango vya usalama.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi, Hassan Saidy amesema baada ya mafanikio makubwa ya kupeleka umeme vijijini, sasa Wakala umefungua ukurasa mpya wa kusambaza huduma za mafuta katika maeneo ambayo kwa muda mrefu hayajapata uwekezaji kutokana na changamoto za kibiashara.

"Wananchi wengi wa vijijini wamekuwa wakinunua mafuta kwa gharama kubwa na wakati mwingine kutoka kwa wauzaji wasio rasmi, jambo linaloongeza hatari za moto pamoja na kupanda kwa gharama za uzalishaji na usafirishaji,"amesema.

Ameongeza kuwa vituo vitakavyojengwa kupitia mpango huo vitafuata sheria, kanuni na viwango vya usalama vilivyowekwa na mamlaka husika ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na salama.

"Wanufaika 8 wa kwanza ndio watakuwa kioo cha mafanikio ya programu hiyo, huku akieleza kuwa serikali imeweka fedha za kutosha kwa ajili ya kuongeza idadi ya vituo vitakavyojengwa katika miaka ijayo," amesema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Nishati Jadidifu na Teknolojia za Nishati Mbadala kutoka REA, Mhandisi Advera Mwijage, alibainisha kuwa zaidi ya shilingi bilioni 12 zimetengwa na Serikali kufanikisha mpango huo kote nchini, ambapo kila mnufaika, ametengewa mkopo wa takribani shilingi milioni 133.

Alieleza kuwa katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, REA imepokea maombi 258, huku waombaji nane wa kwanza wakikamilisha taratibu na kukabidhiwa jumla ya Shilingi bilioni 1, wakati maombi mengine 10 yapo kwenye hatua za mwisho za tathmini.

Naye Mkurugenzi wa Maendeleo ya Biashara wa Benki ya Azania, Yahya Mbanka, alisema benki hiyo imejipanga kutoa usimamizi wa kifedha, elimu ya biashara na ushauri wa kitaalamu kwa wanufaika ili kuhakikisha miradi hiyo inakuwa endelevu na yenye tija kwa jamii.

Mmojawapo wa wanufaika wa kwanza wa mkopo huo, Bwana Boaz Nyakeke, aliishukuru Serikali na kueleza kuwa mradi huo utasaidia kudhibiti bei za mafuta kufuata miongozo ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), jambo litakalowasaidia wakulima, wavuvi na wasafirishaji vijijini.

Serikali imeeleza kuwa dirisha la maombi bado liko wazi kwa wajasiriamali wengine, na katika hatua zinazofuata inaangazia pia uwekezaji wa vituo vya Gesi Asilia (CNG) ili kupanua zaidi wigo wa nishati safi na nafuu nchini.

Post a Comment

Previous Post Next Post