" TIANPING YAIOMBA RADHI SERIKALI YA TANZANIA, YAAHIDI MABADILIKO, SERIKALI YASISITIZA ULINZI KWA WAFANYAKAZI

TIANPING YAIOMBA RADHI SERIKALI YA TANZANIA, YAAHIDI MABADILIKO, SERIKALI YASISITIZA ULINZI KWA WAFANYAKAZI

Kampuni ya Tianping Investment Management Ltd imeomba radhi kwa Serikali ya Tanzania na kuahidi kurekebisha kasoro zote zilizobainika katika mgodi wake uliopo kijiji cha Mhandu, kata ya Segese wilayani Kahama, mkoani Shinyanga, ndani ya siku saba.

Ahadi hiyo ilitolewa na Meneja Mkuu wa kampuni hiyo nchini (Country Manager), Yin Yanqiang, alipofika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Frank Nkinda, kufafanua hatua zinazochukuliwa na kampuni kufuatia ukaguzi wa Kamati ya Usalama ya Wilaya uliobaini ukiukwaji wa sheria za kazi, madini na mazingira.

Yin alisema aliporejea nchini baada ya kutokuwepo wakati kasoro hizo zilipobainika, aliona ni muhimu kukutana na Serikali ya Wilaya ili kuthibitisha dhamira ya kampuni ya kutekeleza maagizo yote yaliyotolewa.

"Ninaahidi tutatekeleza yote tuliyoelekezwa. Tutahakikisha wafanyakazi wote wanapata mikataba ya ajira, vifaa vya kujikinga kazini na muda wa kutosha wa kupumzika. Pia wafanyakazi wa Kichina lazima waheshimu watu wa eneo hili," alisema.

Aliongeza kuwa kampuni imejipanga kukamilisha marekebisho yote ndani ya siku saba kuanzia Julai 14, 2026, huku akiomba radhi kwa kasoro zilizojitokeza.

"Ninaomba radhi kwa mambo yote yaliyotokea. Kampuni yetu itabadilika, na nitafanya kila niwezalo kuhakikisha kila kitu kinakuwa vizuri," alisema.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Frank Nkinda, alisema Serikali imepokea uongozi wa Tianping baada ya ukaguzi kubaini changamoto mbalimbali zilizokuwa zikiwakabili wafanyakazi wa Kitanzania kutokana na kutokuzingatiwa kikamilifu kwa sheria za kazi na madini.

"Tumepokea ugeni kutoka kampuni ya Tianping baada ya ukaguzi tulioufanya na kubaini changamoto mbalimbali ambazo Watanzania walikuwa wanakumbana nazo kutokana na kutokuwepo kwa usimamizi mzuri wa kampuni dhidi ya sheria zetu za kazi na madini," alisema.

Nkinda alisema Serikali iliipa kampuni muda wa siku saba kutekeleza matakwa yote ya kisheria, huku Kamati ya Usalama ikitarajiwa kurejea mgodini baada ya muda huo kujiridhisha na utekelezaji wa ahadi zilizotolewa.

"Baada ya siku saba Kamati ya Usalama itarudi tena kujiridhisha juu ya utekelezaji wa ahadi walizotoa za kutekeleza matakwa ya kisheria ambayo kwa kiasi kikubwa hayakuwa yametekelezwa," alisema.

Alisisitiza kuwa Serikali itaendelea kuwakaribisha wawekezaji wa ndani na nje kwa kuwa ni wadau muhimu wa maendeleo ya uchumi wa Kahama, lakini akaonya kuwa uwekezaji lazima uendane na uzingatiaji wa sheria za Tanzania pamoja na ulinzi wa haki za wafanyakazi.

"Tunawajibika kuwalinda wawekezaji wetu ili waendelee kukua, lakini wakati huohuo tunawajibika kuwalinda Watanzania wanaofanya kazi katika maeneo hayo ili kuimarisha imani yao kwa Serikali," alisema.

 

Post a Comment

Previous Post Next Post