Katika hatua inayolenga kupanua wigo wa utoaji wa elimu kwa umma, timu ya maofisa wa juu kutoka Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) imefanya ziara rasmi katika Makao Makuu ya Muda ya Tanzania Bloggers Network (TBN), yaliyopo Kijitonyama, Dar es Salaam, kwa ajili ya kufanya mazungumzo ya kimkakati na viongozi wa mtandao huo.
Mazungumzo hayo yalilenga kujenga ushirikiano wenye manufaa kwa pande zote mbili, hususan katika masuala ya habari, uelimishaji wa umma na usambazaji wa taarifa na maarifa sahihi kuhusu mifumo ya hifadhi ya jamii, pensheni pamoja na uwekezaji unaofanywa na PSSSF.
Akizungumza katika mkutano huo, Mwenyekiti wa TBN, Beda Msimbe, alisema mtandao huo uko tayari kutumia majukwaa yake kusimama kidete katika kutoa elimu na kusambaza taarifa sahihi kwa umma, hususan kupitia majukwaa ya kidijitali.
Hata hivyo, alisisitiza umuhimu wa wanachama wa TBN kupata mafunzo ya kina kuhusu shughuli, huduma na uendeshaji wa PSSSF, ili waweze kuwaelimisha wananchi kwa ufanisi na kwa usahihi zaidi.
“Ni muhimu kwanza sisi wanachama wa TBN kupata elimu ya kutosha kuhusu mfuko huu, ili elimu tutakayokwenda kuwapa wananchi iwe sahihi, yenye uelewa mpana na yenye tija,” alisema.
Kwa upande wake, Mkuu wa msafara wa PSSSF, Abdul Njaidi, alisema ziara hiyo imelenga kujenga uhusiano wa karibu na wadau wa sekta ya habari, pamoja na kuimarisha juhudi za kutoa elimu kwa jamii kuhusu masuala ya hifadhi ya jamii.
Njaidi aliwahakikishia viongozi wa TBN kuwa hoja na mapendekezo yote yaliyowasilishwa katika mkutano huo yatafanyiwa kazi, akisisitiza kuwa ushirikiano huo unalenga kuhakikisha wananchi wanapata uelewa mpana na sahihi kuhusu masuala ya pensheni na uwekezaji unaofanywa na PSSSF.
Naye Mdhamini wa TBN, Issa Michuzi, alisema mtandao huo wenye historia kubwa katika tasnia ya habari za mtandaoni unajivunia weledi na ufanisi katika kutekeleza majukumu yake.
Alisema TBN ipo kwa ajili ya kuhakikisha Tanzania inasomeka vyema katika medani za kidijitali, kwa kutoa taarifa zenye kujenga na kuchochea maendeleo ya taifa.
“Tunataka kuhakikisha Tanzania inasomeka vyema katika medani za kidijitali na kwamba taarifa zinazotolewa zinakuwa na mchango katika kuchochea na kutanua zaidi gurudumu la maendeleo ya taifa,” alisema Michuzi.
Kwa upande wake, Katibu wa TBN, Rahel Pallangyo, alisema mtandao huo uko tayari kutoa waandishi wake mahiri na kutumia majukwaa yake mbalimbali kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi, za kuaminika na zenye tija kwa jamii.
Alisema ushirikiano huo utasaidia kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu masuala ya hifadhi ya jamii na kuwawezesha wadau mbalimbali kuelewa kwa kina huduma na fursa zinazotolewa na PSSSF.
Ushirikiano huo unatazamiwa kufungua ukurasa mpya katika matumizi ya vyombo vya habari vya mtandaoni katika kufikisha elimu ya hifadhi ya jamii kwa wananchi wengi zaidi nchini.
Katika mkutano huo, ujumbe wa PSSSF ulioongozwa na Abdul Njaidi ulihusisha pia maofisa Regina Kumba, Grayson Mgunda na Doreen Lyimo.
Kwa upande wa TBN, viongozi walioshiriki mkutano huo ni Mwenyekiti Beda Msimbe, Katibu Rahel Pallangyo, Mtaalamu wa Mawasiliano Cathbert Kajuna na Mdhamini wa TBN, Issa Michuzi.

SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254
.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)



.jpeg)

Post a Comment