" TAMASHA LA 19 HIMAYA YA JIGOKU LATOA UJUMBE WA AMANI, MSHIKAMANO NA UTUNZAJI WA MILA

TAMASHA LA 19 HIMAYA YA JIGOKU LATOA UJUMBE WA AMANI, MSHIKAMANO NA UTUNZAJI WA MILA

Ujumbe wa amani, mshikamano na kuheshimu mila na tamaduni za Kitanzania umetawala katika Tamasha la 19 la Himaya ya Jigoku, Masela, Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu, lililoandaliwa na Mwenyekiti wa Machifu Tanzania na Mtemi wa Himaya hiyo, Chifu Antonia Sangalali.

Akizungumza katika tamasha hilo, Chifu Sangalali amewataka wananchi kuendelea kuitunza amani ya Tanzania, kuheshimu Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuzingatia maadili katika maisha ya kila siku.

Amesema matamasha hayo yanayofanyika kila mwaka yakiwa na burudani za ngoma za asili ni sehemu ya kuwaunganisha wananchi, kuendeleza mila na tamaduni pamoja na kutoa elimu mbalimbali kwa jamii.

Chifu Sangalali amesema amani ni msingi wa maendeleo na ustawi wa jamii, hivyo wananchi wanapaswa kuilinda na kuepuka vitendo vinavyoweza kuvuruga utulivu wa nchi.

“Tuendelee kuiheshimu Serikali yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tuendelee kuiweka amani mbele na maadili tuyafuate ili tuweze kuishi kwa amani,” amesema Chifu Sangalali.

Kwa upande wake, mgeni rasmi katika tamasha hilo, Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Dkt. Vicent Anney, amempongeza Chifu Antonia Sangalali kwa kuendelea kuandaa tamasha hilo kila mwaka, akisema limekuwa sehemu muhimu ya kuhifadhi historia, mila na tamaduni za Tanzania.

Amewataka wananchi, hususan vijana, kuendelea kudumisha amani, mshikamano na kuheshimu mila na desturi za Kitanzania.

“Bila utamaduni wetu kuuheshimu taifa litapotea. Ili tuwe na taifa bora lazima tutunze mila na desturi zetu. Niwaombe hasa vijana tutunze amani na mshikamano,” amesema Dkt. Anney.

Baadhi ya wakazi wa Himaya ya Jigoku wamepongeza juhudi za Chifu Sangalali za kuendelea kuandaa tamasha hilo kila mwaka, wakisema limekuwa likiwakutanisha ndugu na jamii kwa ujumla, huku likitoa nafasi ya kubadilishana ujumbe wa amani, maadili na umuhimu wa kutunza mila na tamaduni.

SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA

🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA

  • Wasiliana nasi:
    📍 East African Spirits (T) Ltd
    📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254

Post a Comment

Previous Post Next Post