" SERIKALI YASISITIZA USIMAMIZI ENDELEVU WA RASILIMALIZA MAJI

SERIKALI YASISITIZA USIMAMIZI ENDELEVU WA RASILIMALIZA MAJI

 

Na, Egidia Vedasto, Misalaba Media, Arusha.


Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesisitiza umuhimu wa usimamizi endelevu wa rasilimali za maji kwa ajili ya kuchochea maendeleo ya kiuchumi, kulinda mazingira na kuboresha maisha ya wananchi.


Akizungumza katika ufunguzi wa Kongamano la 27 la WaterNet jijini Arusha, Katibu Tawala wa mkoa wa Arusha Dr. Toba Nguvila akimuwakilisha Waziri mkuu Dr. Mwigulu Nchemba  amewakaribisha washiriki kutoka Afrika Mashariki, Kusini na maeneo mengine duniani, huku akiwapongeza WaterNet na washirika wake kwa kuendeleza jukwaa la kubadilishana maarifa ya kisayansi na kuimarisha ushirikiano wa kikanda.


Amesema maji ni rasilimali muhimu kwa maisha na maendeleo ya uchumi, kwa kuwa yanasaidia shughuli za kilimo, ufugaji, uvuvi, viwanda, nishati, utalii na afya ya umma. Ameeleza kuwa maziwa, mito, maeneo oevu, maji ya chini ya ardhi pamoja na vyanzo vingine vya maji ni rasilimali muhimu zinazopaswa kulindwa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.


Dr. Nguvila amesisitiza kuwa usimamizi mzuri wa rasilimali za maji unaweza kuongeza uzalishaji, kuvutia uwekezaji na kutengeneza ajira, huku akionya kuwa usimamizi usiofaa unaweza kusababisha uharibifu wa mazingira, hasara za kiuchumi na migogoro baina ya watumiaji wa maji.


Hata hivyo ameongeza kuwa,  changamoto hizo zinahitaji ushirikiano wa Serikali, wataalamu, watafiti, sekta binafsi na jamii katika kuhakikisha rasilimali za maji zinalindwa na kutumika kwa ufanisi.


Amesema "Dira ya Maendeleo ya Tanzania ya mwaka 2050 inahitaji upatikanaji wa maji wa uhakika kwa ajili ya kuendeleza sekta za kilimo, viwanda, nishati, madini, utalii na maendeleo ya miji. Amesema uwekezaji katika usimamizi wa maji ni sehemu muhimu ya kufikia malengo ya maendeleo ya taifa na kuhakikisha rasilimali hiyo inawanufaisha wananchi wa sasa na vizazi vijavyo"amesema Dr. Nguvila.


Kwa upande wake Makamu mkuu wa Chuo kikuu cha Nelson Mandela Prof. Maulilio Kipanyula amesema serikali  isisitize umuhimu wa kuimarisha utafiti, elimu, sayansi na ubunifu wa kiteknolojia katika kukabiliana na changamoto za maendeleo, ikiwemo mabadiliko ya tabianchi na usimamizi endelevu wa rasilimali za maji.


Ametoa wito huo katika kongamano la kisayansi lililowakutanisha wataalamu, watafiti na wadau kutoka Afrika Mashariki, Kusini, Kati na maeneo mengine duniani kujadili matumizi ya teknolojia katika kukabiliana na changamoto za maji.

Akizungumza katika hafla hiyo, mwakilishi wa Serikali amesema matumizi ya akili unde (Artificial Intelligence), takwimu kubwa (Big Data) na teknolojia za kidijitali yanaweza kusaidia kuimarisha ustahimilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi na kuboresha usimamizi wa rasilimali za maji.


Aidha  Prof. Kipanyula amesema mabadiliko ya tabianchi yanaongeza shinikizo kwa rasilimali hizo na kuathiri sekta za kilimo, nishati, afya ya umma, mazingira na maendeleo ya uchumi.

Aidha, amezitaka taasisi za elimu ya juu na vituo vya utafiti kuimarisha ushirikiano na jamii pamoja na sekta ya viwanda ili matokeo ya tafiti yatumike kutatua changamoto halisi zinazowakabili wananchi.


Vilevile ameelezea  umuhimu wa kuwekeza kwa vijana katika sayansi, teknolojia na ubunifu, akisema kongamano hilo linatarajiwa kuchochea tafiti za pamoja na kupata suluhisho endelevu katika usimamizi wa rasilimali za maji.


Katika namna hiyo hiyo Mwenyekiti baraza la Chuo kikuu cha sayansi na teknolojia Mbeya  Zakia Hamdani Meghji amesema upatikanaji wa maji safi na salama ni muhimu kwa mwanamke kwa kuwa unapunguza muda na nguvu zinazotumika kutafuta maji, hivyo kumuwezesha kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi, kijamii na maendeleo ya familia.


Amesema upatikanaji wa maji unachangia pia kuboresha afya na usafi wa wanawake na watoto, hususan katika kipindi cha hedhi, wakati wa ujauzito na kujifungua. Kwa hiyo, amesema uwekezaji katika huduma za maji haupaswi kuangaliwa kama suala la msingi la maisha pekee, bali ni hatua muhimu ya kuwawezesha wanawake na kuimarisha ustawi wa jamii.




Post a Comment

Previous Post Next Post