WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga,akizungumza leo Novemba 2,2026 jijini Dodoma wakati akifungua maonyesho ya bidhaa za viwanda na wajasiriamali, kuelekea uzinduzi wa Sera ya Maendeleo Endelevu ya Viwanda ya mwaka 2025 na Sera ya Maendeleo ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati ya mwaka 2003, toleo la 2025.
Na.Mwandishi Wetu- DODOMA
WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga, amesema sekta ya viwanda inatarajiwa kuchangia asilimia 15 ya Pato la Taifa ifikapo mwaka 2050, huku ikilenga kukua kwa wastani wa asilimia tisa kwa mwaka ili kuimarisha uchumi na kuongeza ajira nchini.
Kapinga amesema hayo leo Novemba 2,2026 jijini Dodoma wakati akifungua maonyesho ya bidhaa za viwanda na wajasiriamali, kuelekea uzinduzi wa Sera ya Maendeleo Endelevu ya Viwanda ya mwaka 2025 na Sera ya Maendeleo ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati ya mwaka 2003, toleo la 2025.
Amesema mapitio ya sera hizo yanalenga kuendana na kasi ya maendeleo ya uchumi na biashara nchini, pamoja na kufanikisha matarajio ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ya kujenga uchumi wenye thamani ya dola trilioni moja za Marekani.
“Sekta ya viwanda na biashara ni nguzo muhimu katika kuchochea uchumi wa taifa letu. Ndiyo maana tumefanya mapitio ya sera hizi ili ziendane na kasi ya uchumi na biashara tunayoiendea,” amesema Kapinga.
Amesema maonyesho hayo yanalenga kuwawezesha Watanzania kuona bidhaa zinazozalishwa nchini, kutambua uwezo wa viwanda vya ndani na kuwafahamu wajasiriamali wanaotumia biashara kama chanzo cha kipato na ajira.
Ameeleza kuwa viwanda na biashara ni miongoni mwa sekta zinazotarajiwa kuchangia kwa kiasi kikubwa kufikia malengo ya ajira yaliyowekwa katika mpango wa utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo, hivyo ni muhimu kuimarisha sekta hizo kwa kuwashirikisha wajasiriamali wadogo.
Mhe.Kapinga amezitaka taasisi zilizo chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara kuendelea kuwawezesha wajasiriamali kwa kuwapatia mafunzo na kuboresha ubora wa bidhaa zao, hususan katika hatua za mwisho za uzalishaji, ufungashaji na muonekano wa bidhaa ili ziweze kushindana katika masoko.
Ametaja bidhaa za ngozi kuwa miongoni mwa bidhaa zinazozalishwa na wajasiriamali nchini zenye ubora, lakini akasisitiza umuhimu wa kuboresha hatua za umaliziaji ili kuongeza mvuto na ushindani wake sokoni.
Aidha, amezitaka taasisi ikiwemo Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kuendelea kutoa mafunzo, ushauri na ithibati kwa wajasiriamali, huku akisisitiza kuwa kuwaingia sokoni hakupaswi kuwa mwisho wa msaada wanaopatiwa.
Amesema serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi ya biashara, kufungua fursa za masoko ya ndani na nje ya nchi na kutatua changamoto zinazokabili viwanda ili viendelee kukua, kuongeza uzalishaji na kutoa ajira kwa wananchi.
Mhe.Kapinga amesema kupitia Tantrade, serikali itaendelea kuimarisha fursa za biashara na kuhamasisha matumizi ya chapa ya Made in Tanzania ili kuongeza uelewa wa bidhaa zinazozalishwa nchini na kuwasaidia wafanyabiashara kuingia katika masoko ya kimataifa.
Ameongeza kuwa serikali itaendelea kushirikiana na BRELA kurasimisha biashara, kusajili wafanyabiashara na kuwawezesha kupata leseni na ithibati zinazohitajika, hatua itakayosaidia kupunguza idadi ya biashara zisizo rasmi na kuimarisha ukuaji wa uchumi.
Hata hivyo amewahimiza Watanzania kutembelea maonyesho hayo, akisema ni fursa ya kujionea ubunifu, uwezo na bidhaa zinazotengenezwa na viwanda pamoja na wajasiriamali wa ndani.

Post a Comment