Na Gabon Mariba - Mara
Mkuu wa Mkoa wa Mara, Brigedia Jenerali Evans Alfred Mtambi, ametangaza kuanza kwa maandalizi ya awamu ya pili ya kampeni ya chanjo ya ruzuku na utambuzi wa mifugo mkoani humo, inayolenga kuchanja jumla ya mifugo 3,576,019, huku Serikali ikitoa kiasi cha Shilingi 286,712,000 kwa ajili ya kufanikisha utekelezaji wa zoezi hilo katika mwaka wa fedha 2026/2027.
Akizungumza na waandishi wa habari mkoani Mara Novemba 12, 2026, Brigedia Jenerali Mtambi amesema awamu hiyo inalenga kuchanja ng'ombe 1,278,778, mbuzi na kondoo 979,913 pamoja na kuku 1,317,328, ikiwa ni ongezeko la mifugo 290,393 ikilinganishwa na idadi iliyochanjwa katika awamu ya kwanza.
Amesema katika awamu hiyo ya pili Serikali imetoa dozi za awali 2,503,213 za chanjo kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa kampeni hiyo, huku wafugaji wakitakiwa kuchangia gharama ya Shilingi 500 kwa kila ng'ombe na Shilingi 300 kwa kila mbuzi au kondoo, wakati chanjo ya kuku itatolewa bure.
Mtambi amesema kampeni hiyo ni mwendelezo wa juhudi za Serikali katika kudhibiti magonjwa ya mifugo, kuimarisha afya ya wanyama, kuongeza uzalishaji na kulinda masoko ya mifugo ndani na nje ya nchi.
Ameeleza kuwa katika awamu ya kwanza iliyozinduliwa kitaifa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, mwezi Juni 2025 mkoani Simiyu, Mkoa wa Mara ulipatiwa jumla ya dozi 3,837,500 za chanjo kwa ajili ya ng'ombe, mbuzi, kondoo na kuku, pamoja na vifaa vya utekelezaji vilivyojumuisha vishikwambi 180, pikipiki 28 na hereni za kielektroniki 2,203,300.
Amesema hadi kufikia Julai 2026, jumla ya mifugo 2,209,947 ilikuwa imechanjwa sawa na asilimia 67 ya mifugo 3,285,626 iliyokuwa imepangwa kuchanjwa, ikiwemo ng'ombe 627,578, mbuzi na kondoo 414,459 pamoja na kuku 1,167,910.
Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa Mkoa, kupitia chanjo zilizotolewa katika awamu ya kwanza, Serikali ilikusanya jumla ya Shilingi 438,126,700 kutokana na tozo za chanjo za ng'ombe, mbuzi na kondoo, huku chanjo ya kuku ikitolewa bila malipo.
Aidha, amesema awamu ya pili inatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kupitia tozo za chanjo kwa kiasi kinachokadiriwa kufikia Shilingi 933,362,900.
Katika hatua nyingine, Brigedia Jenerali Mtambi amesisitiza kuwa kampeni hiyo itaambatana na zoezi la utambuzi wa mifugo kwa kutumia hereni za kielektroniki zenye namba maalumu kwa kila mnyama, hatua itakayowezesha Serikali kuwa na takwimu sahihi za mifugo na kufuatilia taarifa zake.
Amesema mfumo huo utakuwa na manufaa kwa wafugaji kwa kuwa utarahisisha upatikanaji wa huduma za bima na mikopo kutoka taasisi za kifedha, pamoja na kuisaidia Serikali kupanga mipango ya maendeleo ya sekta ya mifugo kwa kutumia taarifa sahihi.
Akizungumzia namna zoezi hilo litakavyotekelezwa, amesema timu za wataalamu wa mifugo zitafika katika vijiji na mitaa kutoa huduma za chanjo, huku vituo maalumu vikiandaliwa katika kila Halmashauri ili kuwawezesha wafugaji kupeleka mifugo yao kwa ajili ya kupata huduma hizo.
Ametoa wito kwa wafugaji kufuatilia ratiba na maeneo yatakayotangazwa kupitia viongozi wao wa maeneo husika ili kuhakikisha mifugo yao inapata chanjo na kutambuliwa kwa wakati.
Sambamba na hilo, amewaelekeza Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri pamoja na wataalamu wa mifugo kuhakikisha wanashirikiana kikamilifu kusimamia utekelezaji wa kampeni hiyo, akisisitiza kuwa hatavumilia uzembe wa Halmashauri yoyote katika kutekeleza zoezi hilo muhimu kwa maendeleo ya sekta ya mifugo nchini.
Kampeni hiyo inalenga kudhibiti magonjwa yanayoathiri biashara ya mifugo na afya ya binadamu, huku ikiimarisha uwezo wa Tanzania kukidhi matakwa ya Shirika la Afya ya Wanyama Duniani (WOAH) na kuongeza fursa za kufikia masoko ya kikanda na kimataifa.
PROFESSOR MGOKO EP 07
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254





Post a Comment