Monsinyori Dominic Makalanga Mgata wa Jimbo Katoliki Shinyanga, leo amekiri imani mbele ya Kanisa, ikiwa ni wiki mbili zimepita tangu Baba Mtakatifu Fransisko kumpa hadhi hiyo.
Monsinyori Mgata amekiri imani kupitia Ibada ya Masifu ya Jioni iliyofanyika katika Kanisa kuu la Mama mwenye huruma Ngokolo mjini Shinyanga, ambayo iliongozwa na Askofu wa Jimbo Katoliki Shinyanga Mhashamu Liberatus Sangu, ambayo ilikuwa sehemu ya maandalizi ya utolewaji wa daraja la Ushemasi kwa Frateri Deusdedith Nkandi hapo kesho.
Umonsinyori ni hadhi ya heshima ya pekee ambayo Mapadre wachache hupewa na Baba Mtakatifu kwa mapendekezo ya Askofu wao wa Jimbo, kutokana na mchango mkubwa walioufanya katika utume wa Kanisa.
Jimbo Katoliki Shinyanga kwa sasa lina jumla ya Mapadre watatu wenye hadhi ya Umonsinyori waliopewa heshima hiyo chini ya uongozi wa Askofu Liberatus T.K. Sangu, ambao ni Monsinyori Nobert Ngusa anayefanya utume wake katika Parokia ya Shy bush, Monsinyori Martine Mhango (Mwanamilembe) anayefanya utume wake katika Parokia ya Buhangija na Monsinyori Dominic Makalanga Mgata anayefanya utume wake katika Parokia ya Nyalikungu Maswa
Post a Comment