Askofu wa Jimbo Katoliki Shinyanga Mhashamu Liberatus Sangu, amemtaka Frateri Deusdedith Nkandi anayetarajiwa kupewa daraja la Ushemasi hapo kesho kutoogopa, kwa kuwa ataifanya kazi iliyopo mbele yake kwa maongozi ya Roho mtakatifu.
Askofu Sangu amemtia moyo Frateri Nkandi wakati akitoa homilia katika Ibada ya Masifu ya jioni, ambayo ni maandalizi ya utolewaji wa daraja la Ushemasi hapo kesho, iliyofanyika kwenye Kanisa kuu la Mama mwenye huruma Ngokolo mjini Shinyanga.
Amemtaka kutambua kuwa, Yesu Kristo mwenyewe ndiye aliyemuita na ndiye anayetuma, hivyo anapaswa kwenda kuhubiri neno la Mungu na kutangaza upendo wake kwa maneno na matendo yake huku akiongozwa na roho mtakatifu.
Kupitia Ibada hiyo ambayo pia imehudhuriwa na Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, Shemasi mtarajiwa amekiri imani na kula viapo mbalimbali ikiwemo cha Useja, kufuata sheria na miongozo ya kanisa pamoja na ulinzi wa mtoto.
Kesho Alhamisi, Frateri Nkandi atapewa Daraja la Ushemasi na Mwadhama Kardinali Pengo, kupitia Misa takatifu ambayo itafanyika Kanisa kuu Ngokolo kuanzia saa 4:00 asubuhi.

Post a Comment