" MWENYEKITI WA CCM MKOA WA GEITA AWAPIGIA KELELE WALE WANAOSEMA "NO REFORM NO ELECTION" – ASEMA SAMIA ANA DENI KUBWA GEITA

MWENYEKITI WA CCM MKOA WA GEITA AWAPIGIA KELELE WALE WANAOSEMA "NO REFORM NO ELECTION" – ASEMA SAMIA ANA DENI KUBWA GEITA

Na Mwandishi wetu, Misalaba Media

 Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Geita, Nicholaus Kasendamila, ametoa onyo  kwa watu wanaoeneza kauli ya “No reform, no election” akisema kauli hiyo haina nafasi Geita kwani mchakato wa uchaguzi unaendelea vizuri, huku wananchi wakiendelea kunufaika na utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa kishindo.

Akizungumza na Misalaba Media, Kasendamila amesema baadhi ya watu wanapandikiza hofu kwa wananchi kwa madai yasiyo na msingi, huku wakipuuzia maendeleo makubwa yaliyofanyika chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.

“Wale wanaosema ‘No reform no election’ hayo ni maneno yao, si ya wanaGeita. Huku uchaguzi unaendelea na wananchi wanashiriki kikamilifu. Chama na Serikali tupo salama,” amesema Kasendamila.

Mwenyekiti huyo amesisitiza kuwa Mkoa wa Geita umepewa kipaumbele kikubwa na Serikali ya Awamu ya Sita, hivyo wananchi waendelee kuwa na imani na CCM kwani ndicho chama pekee kinachotekeleza kwa vitendo.

Geita ni miongoni mwa mikoa 26 ya Tanzania Bara iliyoanzishwa mwaka 2012, ikiwa na ukubwa wa kilomita za mraba 28,879. Mkoa huu unaundwa na wilaya tano ambazo ni Geita, Chato, Bukombe, Nyang’wale na Mbogwe, pamoja na halmashauri sita. Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, Mkoa wa Geita una jumla ya watu 2,977,608 wakiwemo wanawake 1,513,844 na wanaume 1,463,764.

Katika kipindi cha utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2020-2025, Geita imepokea jumla ya shilingi bilioni 250 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayogusa sekta mbalimbali kama afya, elimu, barabara, maji, nishati, kilimo, uvuvi, utawala bora na uwezeshaji wa wananchi kiuchumi kupitia asilimia 10 ya mapato ya ndani na mfuko wa TASAF.

“Mafanikio yaliyopatikana Geita ni makubwa sana. Samia ana deni kubwa kwa mkoa huu, lakini anaendelea kulilipa kwa vitendo. Tunawaomba wananchi waendelee kuiamini Serikali ya CCM,” amesema Kasendamila.

Amehitimisha kwa kusema kuwa chama kiko imara na kipo tayari kuendelea kuwatumikia wananchi wa Geita kwa uadilifu na kasi ile ile ya maendeleo.

Post a Comment

Previous Post Next Post