Na Mapuli Kitina Misalaba
Mwalimu
Mondesta Kilasa, akizungumza kwa niaba ya mkuu wa Shule ya Awali na Msingi
Kolandoto katika Manispaa ya Shinyanga, amemshukuru na kumpongeza kijana Moses
Mshagatile kwa moyo wake wa kizalendo baada ya kukabidhi mifuko ya saruji kwa
ajili ya kusaidia ujenzi wa vyoo vya walimu shuleni hapo.
Akizungumza wakati wa tukio hilo, Mwalimu Kilasa
amesema msaada huo umetolewa katika wakati muafaka, kwani kwa muda mrefu shule
hiyo imekuwa ikikabiliwa na changamoto ya ukosefu wa vyoo vya walimu hali
iliyokuwa ikisababisha usumbufu mkubwa kwa walimu.
Kwa upande wake, Moses Mshagatile ambaye ni mzaliwa
wa kata ya Kolandoto na pia ni mmoja wa wanafunzi waliopitia shule hiyo,
amesema ameamua kujitokeza kusaidia baada ya kusikia kupitia vikao vya wazazi
kuwa shule hiyo haina vyoo vya walimu, jambo lililomsukuma kuchangia ili kuweka
mazingira mazuri ya kazi kwa walimu wanaolea kizazi kijacho.
Naye mzazi wa mwanafunzi katika shule hiyo, Sostenes
John, amepongeza hatua ya Moses Mshagatile akisema ni mfano bora wa kuigwa na
vijana wengine, hasa wale waliopitia shule hiyo na wana uwezo wa kusaidia kwa
njia yoyote.
Ujenzi wa vyoo hivyo vya kisasa umeanza hivi
karibuni baada ya uongozi wa shule kukutana na wazazi na wadau wa elimu
kujadili namna ya kushughulikia changamoto hiyo ya muda mrefu.

Moses Mshagatile baada ya kuwasili katika Shule ya
Awali na Msingi Kolandoto uliyopo Manispaa ya Shinyanga, kwa lengo la kukabidhi
msaada wa mifuko ya Saruji.
Moses Mshagatile akisaini kitabu cha wageni katika Shule ya
Awali na Msingi Kolandoto uliyopo Manispaa ya Shinyanga.

Moses Mshagatile akikabidhi mifuko ya Saruji katika Shule
ya Awali na Msingi Kolandoto uliyopo Manispaa ya Shinyanga leo Mei 26, 2025.
Post a Comment