" MKUU WA WILAYA YA SHINYANGA AFUNGA BONANZA LA MALULA HOME TALENTS COMPETITION, ATOA UJUMBE MZITO KUHUSU UCHAGUZI NA VIJANA

MKUU WA WILAYA YA SHINYANGA AFUNGA BONANZA LA MALULA HOME TALENTS COMPETITION, ATOA UJUMBE MZITO KUHUSU UCHAGUZI NA VIJANA

Na Mapuli Kitina Misalaba

Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Wakili Julius Mtatiro, amewahimiza wananchi kuendelea kujiandaa kwa ajili ya kushiriki kikamilifu katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu 2025.

Ametoa wito huo wakati akizungumza  kwenye bonanza la michezo la Malula Home Talents Competition ambalo limefanyika katika uwanja wa Shule ya Msingi Kitangili, Manispaa ya Shinyanga, na kwamba amesisitiza umuhimu wa kujiweka tayari na kupuuza propaganda zisizo na msingi kuhusu uchaguzi huo.

“Uchaguzi umeelezwa kwenye Katiba ya Tanzania kiasi kwamba hata Rais wa nchi hawezi kuzuia uchaguzi usifanyike. Sasa kama Rais hawezi, kuna mtu mwingine anaweza? Hakuna!” amesema Mtatiro kwa msisitizo.

Amesema baadhi ya vijana wamekuwa wakieneza taarifa za kupotosha kuwa hakutakuwa na uchaguzi, jambo ambalo si la kweli, kwani uchaguzi ni haki ya kikatiba inayotekelezwa kila baada ya miaka mitano.

“Tayari maboresho ya daftari la wapiga kura yamekamilika, vyama mbalimbali vimeshaanza maandalizi, na kwa upande wa CCM, mgombea urais ni Dkt. Samia Suluhu Hassan, na mgombea mwenza ni Balozi Dkt. Nchimbi. Wananchi jiandaeni kushiriki uchaguzi huu muhimu kwa mustakabali wa nchi yetu,” amesema.

Katika hatua nyingine, Mtatiro ametumia jukwaa hilo kumpongeza mratibu wa bonanza hilo, Daniesa Malula, kwa juhudi zake katika kuinua vipaji vya vijana kupitia michezo, akimtaja kuwa ni mfano bora wa vijana wenye maono na uthubutu.

“Vijana wengi wanapoteza muda kuangalia TV, kubet au kukaa vijiweni bila kazi. Lakini huyu kijana Malula anajituma kwenye kazi za kijamii. Nakwambia endelea kupambana, hizi kazi zitakulipa baadaye,” amesema Mtatiro.

Baada ya kusikiliza changamoto mbalimbali zilizowasilishwa , zikiwemo mahitaji ya vifaa vya kazi kama kamera ya kisasa yenye thamani ya shilingi milioni mbili, Mtatiro ameahidi kukutana naye ndani ya wiki mbili ili kumsaidia kupata kiasi hicho cha fedha.

Bonanza hilo lililodumu kwa siku kadhaa limehusisha michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa miguu, mbio za baskeli, kuvuta kamba, mashindano ya kula, mashindano ya dansi, maonyesho ya pikipiki pamoja na burudani za ngoma za jadi kutoka maeneo mbalimbali ya Shinyanga.

Post a Comment

Previous Post Next Post