" SERIKALI YAAHIDI KUENDELEA KUBORESHA HUDUMA ZA AFYA KWA WAZEE, KUWALINDA NA KUWEKA MIPANGO MIKAKATI BORA YA KUKOMESHA UKATILI DHIDI YAO

SERIKALI YAAHIDI KUENDELEA KUBORESHA HUDUMA ZA AFYA KWA WAZEE, KUWALINDA NA KUWEKA MIPANGO MIKAKATI BORA YA KUKOMESHA UKATILI DHIDI YAO

Na Elisha Petro, Misalaba Media

Serikali kwa kushirikiana na wadau wa haki za binadamu, imeahidi kuendelea kutunza haki za wazee, ikiwemo kuweka mazingira rafiki katika upatikanaji wa huduma bora za afya.

Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Mhe. Mwanaid Ali Khamis, wakati akizungumza kwenye kilele cha Siku ya Kimataifa ya Kuelimisha na Kupinga Ukatili Dhidi ya Wazee Duniani, ambapo maadhimisho hayo kitaifa yamefanyika katika Mkoa wa Shinyanga.

Naibu Waziri huyo amebainisha kuwa Serikali inatambua mchango wa wazee katika maendeleo ya taifa, hivyo itaendelea kubuni na kuandaa mipango mikakati yenye tija kwa wazee.

"Serikali inaendelea kuhakikisha kundi hili la wazee linapata huduma bora, na miongoni mwa maeneo ambayo serikali inashughulika nayo ni eneo la afya, hasa kupata matibabu bila malipo kwa wazee wasiojiweza, ambapo Wizara yetu inaendelea kuhamasisha kwa kutambua mchango wa wazee na kueneza kampeni ya 'Mpishe Mzee Kwanza Apate Huduma'," amesema Mhe. Mwanaid.

Katika hatua nyingine, Mhe. Mwanaid ametumia maadhimisho hayo kuwasisitiza wazee kutokusita kufika katika vituo vya kutolea msaada wa kisheria kuwasilisha changamoto zinazowakabili katika jamii, ikiwemo dhuruma na unyanyasaji wa kijinsia.

"Niwaombe wazee wangu, Serikali yenu ipo. Siku mzee yoyote atakayedhurumiwa mali zake, usiogope kufika katika ofisi zetu za Serikali. Usikae kimya kwa sababu utapata msongo wa mawazo. Tufike katika ofisi zetu kwa changamoto mbalimbali. Lakini pia nitoe wito kwa jamii kuacha kabisa kufanya matendo yanayoashiria ukatili kwa wazee wetu. Sisi sote tunapaswa kuwalinda, kuwathamini na kuwahudumia wazee wetu, na kila mmoja wetu anapaswa kutoa taarifa sehemu husika atakapoona viashiria vya ukatili ili vishughulikiwe kwa uharaka," amesisitiza Mhe. Mwanaid.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Wakili Julius Mtatiro, amewasisitiza wazazi na walezi kuendelea kuwafundisha vijana stadi mbalimbali za maisha ili kuwajengea uwezo wa kujitegemea baada ya masomo yao.

"Tupunguze sana kasumba ya kulea watu wazima. Wazee mnatakiwa kulelewa. Sasa leo wazazi wanawasomesha watoto kuanzia shule ya msingi hadi chuo kikuu, lakini wale watoto wakimaliza wanarudi kusema 'sisi hatuna ajira, tutunzeni' – no, no, no! Chuoni unaenda kupata ujuzi, siyo ajira. Kijana wako akimaliza chuo kikuu inabidi apambane na maisha. Na sisi wazee tujiwekee mazingira ya kuwafundisha watoto toka wakiwa wadogo," amesema DC Mtatiro.

Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Taifa, David Sendo, ameeleza kuwa Baraza hilo litaendelea kushirikiana ipasavyo na Serikali katika kuhakikisha vitendo vyote vya ukatili kwa wazee, ikiwemo ukatili wa kijinsia, vinakomeshwa.

Naye Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Shinyanga, Luty Masam, amesema Mahakama itaendelea kuwapa kipaumbele wazee ili kuwarahisishia upatikanaji wa haki pindi wanapohitaji msaada wa kisheria.

Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kuelimisha na Kupinga Ukatili Dhidi ya Wazee kitaifa yamekwenda sambamba na kaulimbiu isemayo "Wazee ni hazina kwa taifa, tuwalinde, tuwatunze."

Naibu Waziri Wizara ya Maendeleo ya Jamii,Jinsia,wanawake na makundi maalumu Mwanaidi Khamis akizungumza.

Naibu Waziri Wizara ya Maendeleo ya Jamii,Jinsia,wanawake na makundi maalumu Mwanaidi Khamis akizungumza.

Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro akizungumza.


Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Taifa David Sendo akizungumza.
Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga Flora Kajumla akizungumza.
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga Ruth Masamu akizungumza.

 

Post a Comment

Previous Post Next Post