Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita, amewatoa hofu wananchi wa mkoa huo kuhusu hali ya usalama kuelekea Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025, akisisitiza kuwa mkoa uko salama na hauna tishio lolote la kiusalama.
Akizungumza katika kikao na waandishi wa habari kilichofanyika kwenye ukumbi wa Virgimack Hotel, Mhita amesema Serikali ya Mkoa imejipanga kikamilifu kuhakikisha zoezi la kupiga kura linafanyika kwa amani, utulivu na haki bila bughudha kwa mpiga kura yeyote.
“Natoa rai kwa wananchi wa Shinyanga kujitokeza kwa wingi kutumia haki yao ya kikatiba. Serikali tupo tayari, vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vipo macho kuhakikisha siku hiyo inapita kwa amani. Hakuna tishio lolote la kiusalama,” amesema Mhita.
Amesisitiza kuwa yeyote atakayebainika kuchochea vurugu au vitendo vinavyoashiria uvunjifu wa amani atachukuliwa hatua kali za kisheria mara moja, ili kulinda utulivu wa mkoa na kuhakikisha kila mwananchi anatekeleza wajibu wake bila hofu.
“Tunaendelea kufuatilia kwa karibu mienendo yote ya kisiasa na kijamii. Hatutamvumilia mtu yeyote atakayevuruga amani. Tunataka uchaguzi uwe wa heshima, utulivu na unaoendana na maadili ya taifa letu,” aliongeza.
Aidha, alisisitiza kuwa amani ni msingi wa maendeleo, na kwamba hakuna mkoa au taifa linaloweza kupiga hatua kiuchumi au kijamii pasipo utulivu.
Kwa upande wake, aliwataka waandishi wa habari kushirikiana na Serikali katika kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa kushiriki uchaguzi kwa amani, pamoja na kutoa taarifa sahihi na zinazojenga umoja wa kitaifa.
VIDEO: RC MHITA: SHINYANGA IKO SALAMA, WANANCHI JITOKEZENI KUPIGA KURA KWA AMANI
Misalaba Media
0
Post a Comment