Wakati Taifa likielekea katika kipindi cha Uchaguzi, mjadala mkali umeibuka kuhusu njia bora ya kufikia mabadiliko ya kisiasa, huku baadhi ya wachambuzi wakihimiza Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kujifunza kutoka kwa kiongozi mkongwe wa upinzani nchini Kenya, Hayati Raila Odinga.
Kiini cha mjadala huo, mtandaoni ni kauli iliyozungumzwa na mmoja wa wachambuzi wa masuala ya kimataifa na siasa ndugu Majid Mjengwa wakati akihojiwa na mmoja ya vyombo vya habari nchini .
Ilielezwa na Majid kuwa mshauri huyo wa karibu wa Chadema, ameonesha kwamba uvumilivu na kufuata utaratibu ndio suluhishi la mizozo na huonesha ukomavu wa kisiasa, na kwamba mazungumzo ndiyo yanayoleta mabadiliko na si vurugu.
Washiriki waliochangia katika mtandao wengi wao walisisitiza umuhimu wa Chadema kutanguliza majadiliano, wakimtumia Odinga kama mfano wa kiongozi aliyekuwa karibu na upinzani wa Tanzania na ambaye, kulingana na wao, alishika falsafa ya majadiliano katika siasa.
Hata hivyo, mijadala ya mtandaoni inaonyesha maoni yaliyogawanyika kuhusu rekodi ya Odinga na mbinu anazopaswa Chadema kuiga. Baadhi wanaeleza kuwa licha ya Odinga kuwa mshauri, historia yake ya kisiasa pia inajumuisha matukio ya kususia Uchaguzi na kujiapisha kama 'Rais wa wananchi' baada ya Mahakama Kuu kuamuru Uchaguzi urudiwe, hatua iliyofuatiwa na vurugu na maafa. Wanaona matukio haya kama mifano ya kuepukwa, wakisisitiza kuwa kususia Uchaguzi si suluhisho.
Mjadala pia uliibua hoja kuhusu msimamo wa Odinga mwenyewe, akitajwa kuwa alihimiza Wakenya kuandamana. Wengine wanahoji iwapo, baada ya matukio hayo, Odinga mwenyewe alishika Nchi.
Licha ya utata huo, jumbe nyingi zinaweka mkazo katika wito wa ukomavu. Mchambuzi mmoja anahoji kuwa hali ya kukosekana kwa mazungumzo kati ya Chadema na watawala imekuwa changamoto, ingawa anakiri kwamba suala la siasa za Afrika na historia ya viongozi wake (kama vile Odinga kuhukumiwa kwa uhaini na kisha kukubali mazungumzo kwa maslahi ya Taifa) ni elimu tosha.
Mwisho wa yote, jumbe hizo zinahitimisha kwa ujumbe mmoja mkuu, kama inavyoelezwa: "Demokrasia mahala ambapo hakuna uvumilivu haiwezi kuota mizizi." Ujumbe huu unasisitiza haja ya viongozi na wafuasi wa kisiasa kukumbatia uvumilivu, kufuata taratibu za kikatiba na Sheria, na kutanguliza mazungumzo kama njia kuu ya kutatua migogoro na kuleta mageuzi nchini.
Post a Comment