" WATANZANIA WAISHIO MAREKANI WAMUUNGA MKONO RAIS SAMIA

WATANZANIA WAISHIO MAREKANI WAMUUNGA MKONO RAIS SAMIA

Watanzania wanaoishi Marekani wamejitokeza kwa wingi kuunga mkono Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, huku wakilaani vikali uchochezi unaofanywa na mwanaharakati wa mtandaoni, Mange Kimambi, wanaomtuhumu kutumia mitandao kujaribu kuichafua nchi na kupandikiza chuki kwa Watanzania.

Kwenye mahojiano maalum na waandishi wetu kupitia simu na majukwaa ya kijamii, Watanzania hao wametoa sauti moja ya amani, mshikamano, na maendeleo wakisisitiza kuwa hakuna sababu yoyote ya vurugu nchini Tanzania, ambayo kwa sasa inatajwa kuwa miongoni mwa nchi salama na zenye uchumi imara barani Afrika.

Arnold Kaira, Mtanzania anayeishi Texas kwa zaidi ya miaka 10, alisema kwa hasira: “Rais anafanya kazi kubwa ya maendeleo. Tunaona upanuzi wa miundombinu, sera za uwekezaji na uchumi unaokua. Kwa nini tutake kuvuruga haya yote? Huyu dada anayetaka machafuko achunguzwe, anaonekana kutumika na maadui wa nchi yetu.”

Naye Bi. Maria Kapinga, mfanyabiashara kutoka Washington DC, aliongeza: “Maandamano anayoyahamasisha Mange hayana msingi. Tanzania inapiga hatua, barabara, viwanja vya ndege, elimu bure, huduma bora za afya. Tunajivunia nchi yetu, siyo kuiharibu.”

Kwa upande wake, mwekezaji kutoka California, Joseph Bamba, alisisitiza kuwa uchochezi huo ni tishio kwa uwekezaji: “Serikali ya Rais Samia imeweka mazingira bora kwa wawekezaji. Tunaona ukuaji katika sekta ya kilimo, utalii na uchumi wa buluu. Uchochezi huu ni hatari kwa mustakabali wa maendeleo.”

Aidha, mwalimu na mfanyabiashara Bi. Lillian Mushi kutoka New York, aliongeza: “Kama mama na mwalimu, ninaona juhudi kubwa za Serikali katika elimu na afya. Mange anataka kuharibu haya yote. Sisi Watanzania wa Marekani tunasema hapana amani kwanza, maendeleo mbele.”

Mwakilishi wa Ubalozi wa Tanzania Marekani (ambaye hakutaka jina litajwe) alithibitisha kuwa siku ya maandamano yaliyodaiwa kufanyika Oktoba 17, walijitokeza watu wachache tu, bila sapoti yoyote kutoka jamii ya Watanzania walioko Marekani: “Watanzania wa hapa wanaelewa kinachoendelea nyumbani. Wanashiriki kukuza picha chanya ya Tanzania, siyo kuichafua.”

 

Post a Comment

Previous Post Next Post