WAZIRI wa Nishati, Mhe. Deogratious Ndejembi,akizungumza wakati akifungua Baraza Kuu la 55 la Wafanyakazi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) leo Januari 22,2026 jijini Dodoma.

WAZIRI wa Nishati, Mhe. Deogratious Ndejembi,akizungumza wakati akifungua Baraza Kuu la 55 la Wafanyakazi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) leo Januari 22,2026 jijini Dodoma.



SEHEMU ya washiriki wakimsikiliza Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratious Ndejembi, wakati akifungua Baraza Kuu la 55 la Wafanyakazi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) leo Januari 22,2026 jijini Dodoma.

MKURUGENZI Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Bw. Lazaro Twange,akizungumza wakati wa Baraza Kuu la 55 la Wafanyakazi wa TANESCO lililofunguliwa na Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratious Ndejembi leo Januari 22,2026 jijini Dodoma.

WAZIRI wa Nishati, Mhe. Deogratious Ndejembi,akiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kufungua Baraza Kuu la 55 la Wafanyakazi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) leo Januari 22,2026 jijini Dodoma.
Na.Alex Sonna,DODOMA
WAZIRI wa Nishati, Mhe. Deogratious Ndejembi, amelipongeza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa hatua kubwa za kuboresha huduma kwa wateja, akisema mageuzi yanayoendelea ndani ya Shirika hilo yanadhihirisha dhamira ya dhati ya kuimarisha upatikanaji wa umeme na kuongeza ufanisi.
Akizungumza leo Januari 22,2026 jijini Dodoma wakati akifungua Baraza Kuu la 55 la Wafanyakazi wa TANESCO,Waziri Ndejembi amesema kuwa maboresho yanayofanywa na Shirika yametoa matumaini mapya kwa wananchi na kuimarisha utendaji.
Miongoni mwa maboresho aliyoyataja ni pamoja na kuimarishwa kwa mifumo ya mawasiliano kwa wateja kupitia WhatsApp Sogozi na Bulk SMS, hatua inayowezesha taarifa muhimu kufikishwa kwa wakati na kupunguza usumbufu.
Aidha, Waziri amesema uzinduzi wa namba 180, huduma ya kupiga bila malipo, umeleta urahisi mkubwa kwa wananchi kutoa malalamiko au kupata msaada wa haraka.
Ameongeza,kuwa matumizi ya mita janja (Smart Meters) na mpango wa “Konekti Umeme – Pika kwa Umeme” kwa wateja na wafanyakazi ni mageuzi yanayoongeza uhalisia wa matumizi, kupunguza usumbufu na kuimarisha udhibiti wa mapato.
“Hatua hizi zinaonyesha wazi kwamba TANESCO ipo katika mwelekeo sahihi wa kuboresha huduma na kupunguza upotevu wa mapato. Huu ni ushahidi wa nia njema ya uongozi wa Shirika katika kutatua kero za wananchi,” amesema Waziri Ndejembi.
Katika hatua nyingine, Waziri Ndejembi amesisitiza umuhimu wa TANESCO kuhakikisha upatikanaji wa umeme wa kutosha na wa uhakika ili kuwezesha mkakati wa Serikali wa kuijenga Tanzania ya viwanda.
“Ili azma hii ya serikali iweze kufikiwa ni rai yangu TANESCO ifanye jitihada za makusudi ili kuhakikisha inazalisha umeme wa kutosha, kuhakikisha miundombinu ya kusafirisha na kusambaza umeme inaboreshwa wakati wote ili kuhakikisha viwanda vinakuwa na umeme wa uhakika na wa gharama nafuu wakati wote,”alisema Amesema, hali hiyo itasaidia kuvutia wawekezaji wengi kwenye sekta ya viwanda na sekta zingine hivyo kuendelea kukuza uchumi wa nchi na kutekeleza Mkakati wa Tanzania ya Viwanda kwa vitendo.
Amesema, Serikali imeazimia kukuza uchumi wa nchi kwa kutengeneza mazingira bora yatakayowezesha ujenzi wa viwanda vingi vya aina zote unafikiwa nchini. Aidha, amesema hatua hiyo itasaidia kuchochea shughuli nyingi za kiuchumi, kama vile kilimo kwa ajili ya kupata malighafi pia itaongeza shughuli za usafirishaji hivyo kuongeza ajira na kipato kwa wananchi.
Waziri huyo ameihakikishia TANESCO ushirikiano wa Serikali katika kukamilisha miradi mikubwa ya umeme, ikiwemo ile ya Gridi Imara na Nishati Jadidifu, ili kuboresha zaidi hali ya umeme nchini.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Bw. Lazaro Twange, amesema Shirika linamshukuru Rais Samia Suluhu Hasan, kwa kuridhia nyongeza ya mshahara na motisha hali ambayo imeongeza utulivu kwa wafanyakazi kuendelea kujituma kuhudumia wananchi.
Baraza hilo linatarajiwa kujadili masuala mbalimbali ya kiutendaji, ustawi wa wafanyakazi na mikakati ya kuimarisha huduma za Shirika kwa wananchi.
Post a Comment