" MAHAKAMA YA WILAYA YA CHUNYA IMEJIPANGA KUMALIZA MASHAURI YOTE NDANI YA MUDA

MAHAKAMA YA WILAYA YA CHUNYA IMEJIPANGA KUMALIZA MASHAURI YOTE NDANI YA MUDA

Na mwandishi wetu, Misalaba Media ChunyaHakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Chunya, Mhe. James Julius Mhanusi, amesema Mahakama ya Wilaya ya Chunya kwa mwaka huu wa mahakama imejipanga kuhakikisha inamaliza mashauri yote yatakayofunguliwa ndani ya mwaka, jambo litakaloifanya kumaliza mwaka bila kuwa na shauri lolote lililosalia.Mhe. Mhanusi ametoa kauli hiyo mapema Februari 02, 2026 katika viwanja vya Msufini vilivyopo Kata ya Lupa, Tarafa ya Kipembawe, wakati wa maadhimisho ya kilele cha Wiki ya Sheria Nchini.Amesema kuwa mwaka jana Mahakama ya Wilaya ya Chunya ilihama na mashauri machache sana, huku Mahakama za Mwanzo zikihama bila shauri hata moja. Alifafanua kuwa mashauri sifuri maana yake ni kwamba mashauri yote yaliyofunguliwa katika Mahakama za Mwanzo wilayani Chunya yalimalizika ndani ya mwaka husika.“Hivyo basi, na sisi Mahakama ya Wilaya tumejipanga kuhakikisha tunamaliza mwaka huu tukiwa tumesikiliza na kumaliza mashauri yote, tofauti na mwaka uliopita ambapo Mahakama ya Wilaya ilihama na mashauri 73,” alisema Mhe. Mhanusi.Aidha, Mhe. Mhanusi amesema kuwa katika kuadhimisha kilele cha Wiki ya Sheria, walitembelea wagonjwa waliokuwepo katika Kituo cha Afya cha Lupa na kuwakabidhi vitu mbalimbali kama ishara ya kuwajali na kushiriki nao katika kipindi chao cha uuguzi. Alisema tendo hilo linapaswa kuwa funzo kwa jamii kuwajali wengine kutokana na kidogo ambacho Mungu amewajalia.Kwa upande wake, Bi. Kissa Ngoloke kutoka TAKUKURU Wilaya ya Chunya, amewataka wananchi wa Chunya kuwa wazalendo na wenye maadili katika maeneo yote. Alisema kuwa mambo hayo mawili yana mchango mkubwa katika mapambano dhidi ya rushwa, huku akisisitiza kuwa rushwa ni adui mkubwa wa haki. Amewahimiza wananchi kuendelea kupambana na rushwa kwa nguvu zote.Naye Wakili wa Kujitegemea, Mhe. Jacqueline Massawe, aliyemwakilisha Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), amewataka wananchi wa Chunya kuendelea kuwatumia na kuwaamini mawakili katika shughuli zao mbalimbali. Alisema hatua hiyo itasaidia kulinda haki zao na kuchochea maendeleo ya mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.Sherehe za kilele cha Wiki ya Sheria Nchini zimeadhimishwa kwa kufanya shughuli mbalimbali zikiwemo utoaji wa elimu ya sheria kwa wananchi, matendo ya huruma pamoja na shughuli nyingine. Katika Wilaya ya Chunya, sherehe hizo zimefanyika Kata ya Lupa, eneo la Msufini, huku kauli mbiu ya maadhimisho hayo ikiwa ni “Mchango wa Mahakama katika Maendeleo ya Taifa.”

 

Post a Comment

Previous Post Next Post