" MAPINDUZI YA RELI YA SGR NA UPANUZI WA BANDARI: KITOVU CHA USAFIRISHAJI

MAPINDUZI YA RELI YA SGR NA UPANUZI WA BANDARI: KITOVU CHA USAFIRISHAJI

Ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) umepiga hatua kubwa, ambapo hadi Desemba 2025 utandazaji wa reli umefikia kilomita 747, sawa na asilimia 61 ya lengo. 

Kauli hiyo imetolewa na Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwwa wakati akizungumza na waandishi wa habari akijibu hoja ya kusuasua kwa ujenzi.

Alisema hakuna kusuasua kwa ujenzi kwani vipande vya Dar es Salaam hadi Morogoro na Morogoro hadi Makutupora vimekaribia kukamilika kwa zaidi ya asilimia 98. Huduma tayari zimeanza kati ya Dar es Salaam na Dodoma, zikipunguza muda wa safari kwa kiasi kikubwa.

Uendeshaji wa SGR umeleta tija kubwa, ambapo abiria milioni 4.6 na tani 52,305 za mizigo zimesafirishwa hadi mwishoni mwa 2025. Mradi huu pia umezalisha ajira zaidi ya 200,000 kwa Watanzania katika nyanja mbalimbali. Shirika la Reli (TRC) sasa limeanza kujiendesha bila ruzuku ya mishahara kutoka serikalini, jambo ambalo ni mafanikio ya kipekee.

Sambamba na reli, Serikali imewekeza katika upanuzi wa Bandari ya Dar es Salaam ili kuongeza uwezo wa kuhudumia tani milioni 50 kwa mwaka. Mradi huu unahusisha ujenzi wa magati 10 mapya na matenki makubwa ya mafuta. Maboresho haya yanalenga kupunguza muda wa meli kukaa bandarini na kuongeza ufanisi wa kikanda.

Aidha, ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo umeanza kwa ajili ya kuhudumia meli kubwa za kisasa (Mega Max). Bandari hii itasaidia kupunguza msongamano katika Bandari ya Dar es Salaam na kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha usafirishaji Afrika Mashariki. Hii ni sehemu ya mkakati wa kufanya sekta ya maji kuchangia zaidi katika uchumi.

Katika maziwa makuu, Serikali imekamilisha ujenzi wa meli mpya kama MV New Mwanza yenye uwezo wa kubeba abiria 1,200. Pia, meli mbili mpya za mizigo zimejengwa katika Ziwa Tanganyika ili kuchochea biashara na nchi ya DRC. Meli ya MT Sangara nayo imekarabatiwa na kuanza safari za kusafirisha mafuta.

Mapato ya bandari yameongezeka kwa kiasi kikubwa baada ya maboresho na mikataba mipya ya uendeshaji. Takwimu za TRA zinaonyesha mapato ya forodha yamefikia shilingi trilioni 8.256, likiwa ni ongezeko la trilioni 1.17 ikilinganishwa na mwaka uliopita. Ukuaji huu unatokana na kuongezeka kwa ufanisi katika kuhudumia shehena.

Uunganishaji wa SGR na bandari ni mkakati wa kihistoria wa kuimarisha biashara na nchi zisizo na bandari. Reli ya TAZARA nayo inafanyiwa maboresho makubwa kwa kushirikiana na serikali ya Zambia na kampuni ya CCECC. Miradi hii kwa pamoja inaiweka Tanzania katika nafasi bora ya ushindani wa kibiashara kimataifa.







 

  • Wasiliana nasi:
    📍 East African Spirits (T) Ltd
    📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254


Post a Comment

Previous Post Next Post