Na Lydia Lugakila
Mbeya
Mkurugenzi wa WWK Jimbo la Mbeya Kati, Mchungaji Sevelina Luvanda, amewahimiza wanawake wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG) kuyaishi mema yanayompendeza Mwenyezi Mungu, ikiwemo kufanya matendo ya huruma, wanapohitimisha Siku Kuu ya Wanawake Kitaifa.
WWK katika kanisa la TAG inamaanisha Wamama/Wanawake wa Kanisa ambapo ni idara maalum inayolenga kuwaunganisha wanawake wote ndani ya kanisa, kuwakuza kiroho, na kuwajengea uwezo katika nyanja mbalimbali za maisha.
Idara hiyo inalenga kuwafanya wanawake kuwa jeshi la Bwana lenye nguvu, kueneza Injili, na kutimiza Agizo Kuu kwa vitendo pamoja na mali zao.
Bi. Luvanda ametoa kauli hiyo alipokuwa akizungumza na Misalaba Media, akisema kuwa katika kuungana na wanawake wenzao wa TAG Tanzania nzima, wanawake wa Jimbo la Mbeya kati wanapaswa kuzingatia mambo muhimu yanayotakiwa katika wiki ya maadhimisho hayo.
Ameeleza kuwa ni muhimu kutoa ushirikiano kwa wanawake wenzao katika shughuli mbalimbali za wiki hiyo, ikiwemo kushiriki kwaya, kuwatembelea wagonjwa hospitalini, pamoja na kuwatembelea wafungwa, kwa lengo la kumpa Mungu utukufu na kutekeleza kwa dhati shughuli za kijamii.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa wanawake kufanya vizuri katika utoaji wa zawadi kwa watumishi wa Mungu na kutoa sadaka bora siku ya Jumapili, akieleza kuwa hayo ni miongoni mwa malengo yao kulingana na mwongozo wa WWK.
Bi. Luvanda ameongeza kuwa wanawake wanatakiwa kujitoa kwa bidii katika kuinua mfuko wa WWK kitaifa, kijimbo na katika ngazi ya sehemu, ili Mungu aachilie baraka nyingi katika uzao na maisha yao kwa ujumla.
Pia amewapongeza wanawake wa idara ya WWK kwa mafanikio waliyoyapata, akibainisha kuwa wengi wao wameinuka kiuchumi, biashara zao zimekua, watoto wao wamesoma hadi vyuo vikuu, na ndoa zao zimestawi.
Amewakumbusha akina mama kuwalea watoto katika njia ipasayo ili wajifunze neno la Mungu na kutembea katika maadili ya ki Mungu.
Hata hivyo, amesema kupitia idara hiyo ya WWK, wanawake wamefanikiwa kwa kiwango kikubwa, ambapo watoto wao wamepata ajira, wameoa na kuolewa, na wamekuwa baraka kwa kanisa, familia na Taifa.
Aidha,amesema kuwa kupitia idara hiyo wanawake hao wamepata mafunzo kuhusu miradi ya maendeleo, wamejipatia vipato, na hivyo kusaidia familia zao bila kuwa mzigo kwa waume zao.

Post a Comment