
Na. John Bukuku – Dar es Salaam
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Jamhuri ya Uganda, Mhe. Yoweri Kaguta Museveni, wamekubaliana kuimarisha ushirikiano wa matumizi ya bandari, biashara na miundombinu ya usafirishaji ili kurahisisha shughuli za kiuchumi kati ya mataifa hayo mawili na ukanda wa Afrika Mashariki.
Wamebainisha hayo wakati wa mazungumzo ya pamoja ya kuwasilisha ujumbe wa Tanzania na kupokea ujumbe wa Uganda ulioongozwa na Rais wa Jamhuri ya Uganda, Mhe. Yoweri Kaguta Museveni, katika viwanja vya Ikulu jijini Dar es Salaam tarehe 07 Februari, 2026.
Rais Samia amesema kuwa Tanzania itaendelea kutoa fursa kwa Uganda kutumia bandari zake, hususan Bandari za Dar es Salaam na Tanga, kwa usafirishaji wa mizigo, hatua inayolenga kusaidia nchi zisizo na bahari kupata huduma za usafiri wa majini kwa ufanisi zaidi.
Aidha, amebainisha kuwa mpango wa ujenzi wa reli ya Tanga hadi Musoma utarahisisha usafirishaji wa mizigo kupitia Ziwa Victoria kuelekea Uganda, jambo litakalopunguza gharama na muda wa usafiri wa bidhaa.
Pia ameongeza kuwa maendeleo ya reli ya kisasa ya SGR inayotarajiwa kufika Isaka na Lusahunga yatafungua fursa zaidi kwa Uganda kuunganisha miundombinu yake ya reli, hivyo kurahisisha biashara na usafirishaji wa mizigo ndani ya ukanda huo.
Katika kuimarisha biashara, Rais Samia amesema kuwa juhudi zinaendelea kuondoa vikwazo vya kibiashara vinavyokwamisha ukuaji wa soko la Afrika Mashariki ili kuruhusu bidhaa zinazozalishwa ndani ya nchi wanachama kupata soko la uhakika.
Aidha, amebainisha kuwa ushirikiano katika uzalishaji wa nishati kupitia miradi ya pamoja na miradi midogo midogo utasaidia kukuza shughuli za uzalishaji na kuongeza ufanisi wa viwanda na huduma katika mataifa hayo mawili.
Kwa upande wake, Rais Museveni amesema kuwa maendeleo ya uchumi wa Afrika yanategemea uwezo wa mataifa yake kuzalisha mali na huduma pamoja na kuwa na masoko ya uhakika ya bidhaa hizo.
Aidha, amebainisha kuwa usalama wa kikanda ni nguzo muhimu katika kulinda maendeleo ya kiuchumi na biashara, hivyo kuna umuhimu wa kuweka mikakati ya pamoja ya kiusalama katika ukanda wa Maziwa Makuu na Afrika Mashariki kwa ujumla.

🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254
Post a Comment