Mbunge wa Jimbo la Tunduru Kusini, Fadhili Chilombe, ametoa onyo kali kwa watendaji wa Chama Kikuu cha Ushirika Tunduru (TAMCU) kufuatia tuhuma za wizi na udanganyifu uliosababisha zaidi ya shilingi milioni 70 kulipwa kufidia hasara iliyoachwa na baadhi ya makarani wasiokuwa waaminifu.Hatua hiyo imejiri katika ziara ya mbunge huyo alipotembelea TAMCU kufuatia malalamiko ya wakulima waliodai kutolipwa fedha zao kwa wakati licha ya mfumo wa malipo kuonyesha kuwa tayari wamelipwa. Ziara hiyo ilifichua kile kilichoelezwa kuwa mtandao wa vyeti hewa na uingizaji wa majina bandia kwenye mfumo wa ushirika, hali iliyosababisha chama kulazimika kulipa zaidi ya shilingi milioni 70 kufidia hasara.Mwenyekiti wa Ushirika, Mussa Manjaule, alikiri kuwepo kwa changamoto hiyo akisema kuwa ingawa mizani ya kidijitali imeleta uwazi mkubwa katika upimaji wa mazao na kuhakikisha mkulima hapunjwi, bado baadhi ya watendaji wamekuwa wakitumia vibaya utaratibu wa uandikaji wa vyeti. Alisisitiza kuwa tatizo si mfumo bali ni kukosekana kwa uadilifu kwa baadhi ya watendaji.Kwa upande wake, Meneja wa TAMCU, Marcelino Mrope, alieleza kuwa baadhi ya makarani wamekuwa wakiandika vyeti kwa majina ya ndugu au marafiki bila mzigo halisi kuwepo galani. Katika mazingira hayo, tani huonekana kwenye mfumo ilhali hazipo, na fedha hulipwa kwa majina yasiyo halali huku mkulima anayestahili akibaki akidai malipo yake.Uchunguzi wa ndani unaonyesha kuwa baadhi ya makarani hulipwa takribani shilingi laki mbili kwa msimu wa miezi mitatu hadi minne, jambo linalotajwa kuwa chanzo cha baadhi yao kutafuta njia zisizo halali za kujiongezea kipato. Hata hivyo, viongozi wa chama wamesisitiza kuwa mishahara midogo haiwezi kuwa sababu ya kuhalalisha wizi wa fedha za wakulima.Akizungumza katika ziara hiyo, Chilombe alisisitiza kuwa fedha za ushirika haziwezi kuendelea kutumika kulipia upungufu uliosababishwa na mtu mmoja au kikundi cha watu. Alitaka mifumo ya kielektroniki iimarishwe zaidi, ikiwemo ufuatiliaji wa mzigo kuanzia unapoletwa hadi unaposafirishwa, ili kuondoa mianya ya udanganyifu na kurejesha imani ya wakulima kwa chama chao.Ziara hiyo imeacha ujumbe mzito kwa watendaji wa ushirika Tunduru kuwa uwajibikaji ni lazima na si hiari. Wakulima wanahitaji malipo yao kwa wakati na kwa usahihi, na sasa macho yote yameelekezwa kwenye utekelezaji wa maagizo na mapendekezo yaliyotolewa ili kuzuia kurudiwa kwa kashfa hiyo katika misimu ijayo.




🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254






Post a Comment