Na Mapuli Kitina Misalaba
Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) ni taasisi
muhimu ya Serikali iliyoanzishwa kwa mujibu wa The Executive Agencies Act,
Sura ya 245, kwa lengo la kusimamia rasilimali za misitu na nyuki nchini
kwa ufanisi na tija.
Kuanzishwa kwa TFS kulikuja baada ya mageuzi ya
kisekta ambapo mwaka 2009 kulikuwepo Idara ya Misitu na Nyuki (FBD), kabla ya
kuanzishwa rasmi kwa TFS mwaka 2010/11. Baadaye, majukumu yake yalipanuliwa
mwaka 2018 na 2019 kwa kujumuisha shughuli za TTSA na vituo vya malikale
kupitia Tangazo la Serikali Na. 269 (GN 269).
Taasisi hii inaongozwa na sera na sheria mbalimbali
ikiwemo Forest and Beekeeping Policy ya mwaka 1998, pamoja na Sheria
ya Misitu Sura ya 328 na Sheria ya Ufugaji Nyuki Sura ya 224.
Dira ya TFS ni kuwa kinara barani Afrika katika
usimamizi endelevu wa rasilimali za misitu na nyuki, huku dhima yake ikiwa ni
kulinda, kuendeleza na kutumia rasilimali hizo kwa manufaa ya kizazi cha sasa
na kijacho.
Kwa ujumla, Tanzania ina takribani hekta milioni 48.1
za misitu, ambapo sehemu kubwa ipo chini ya usimamizi wa serikali za vijiji na
serikali kuu. TFS pekee inasimamia misitu 464 yenye jumla ya hekta milioni
14.5, ikiwemo misitu ya asili, mashamba ya miti, mikoko pamoja na hifadhi za
nyuki.
Shamba la miti la Sao Hill ni moja ya miradi mikubwa
na ya kimkakati inayosimamiwa na TFS. Shamba hili lina historia ndefu iliyoanza
na majaribio ya upandaji miti kati ya mwaka 1939 hadi 1951, kabla ya kuanza
upandaji mkubwa kuanzia mwaka 1960 hadi 1980.
Mhifadhi Mkuu wa Shamba la Miti Sao Hill - PCO Tebby
Yoramu alifafanua kuwa shamba hilo lipo katika maeneo ya Mufindi mkoani Iringa
na Kilombero mkoani Morogoro, na linajumuisha jumla ya misitu 13 ya hifadhi
yenye eneo la hekta 135,903. Kati ya hizo, zaidi ya hekta 86,000 ni mashamba ya
miti yaliyopandwa, huku sehemu iliyobaki ikiwa ni misitu ya asili na maeneo ya
uwekezaji.
PCO Tebby Yoramu alisema Kiutawala shamba hilo
limegawanywa katika tarafa nne ambazo ni Irundi, Ihefu, Ihalimba na Mgololo,
kila moja ikiwa na majukumu ya kusimamia uzalishaji na ulinzi wa misitu.
Msaidizi wa Mhifadhi Mkuu wa Shamba la Miti Sao Hill
anayesimamia Mipango na Matumizi ya Rasilimali Misitu - SCO Peter Nyahende alisema
shughuli zinazofanyika Sao Hill ni pamoja na: Maandalizi ya upandaji miti, Uzalishaji
wa miche, usimamizi wa Bustani, Upandaji, upaliliaji (weeding), upogaji
(pruning) na upunguzaji miti (thinning)
Shughuli zingine ni Ulinzi wa misitu dhidi ya moto, uvamizi,
Ukusanyaji wa mapato ya serikali na Ushirikishwaji wa jamii katika uhifadhi
ambapo Zaidi ya hayo TFS imekuwa ikishirikisha jamii zinazozunguka shamba hilo
ili kunufaika kiuchumi kupitia ajira, biashara ndogo ndogo na miradi ya kijamii
jambo linalochochea ulinzi wa rasilimali hizo.
Katika kuimarisha uelewa wa jamii kuhusu umuhimu wa
rasilimali za misitu na fursa zake kiuchumi, viongozi na wanachama wa Taasisi
ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Jangwa la Sahara, Tawi la Tanzania (MISA TAN),
ambao ni waandishi wa habari na watangazaji kutoka vyombo mbalimbali nchini,
walifanya ziara mkoani Iringa kutembelea maeneo ya utalii na uzalishaji,
ikiwemo Shamba la Miti la Sao Hill linalosimamiwa na Tanzania Forest Services
Agency (TFS).
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mkuu wa Mkoa wa
Iringa, Kheri James alisema kuwa mkoa huo una fursa nyingi za kiuchumi pamoja
na vivutio vya utalii vinavyohitaji kutangazwa zaidi ili kuvutia wawekezaji na
kuongeza mchango wake katika uchumi wa taifa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa MISA Tanzania, Edwin
Soko alisema ziara hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa kauli mbiu ya kongamano lao
la Mwaka 2026 isemayo “Iringa Imara Itajengwa kwa Umoja na Uwajibikaji,”
akisisitiza nafasi ya vyombo vya habari katika kuelimisha umma kuhusu uhifadhi
wa misitu na matumizi endelevu ya rasilimali.
Baadhi ya waandishi wa habari walioshiriki ziara hiyo
akiwemo Moshi Ndugulile, Simeo Makoba, Amina Mbwambo, Kadama Malunde, Neema
Nkumbi na Marco Maduhu, walieleza kuwa ziara hiyo imewapa uelewa mpana kuhusu
mchango wa misitu katika uchumi na umuhimu wa kuelimisha jamii juu ya uhifadhi
wake.
Mbali na ziara hiyo, Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa
wa Shinyanga (Shinyanga Press Club – SPC) ilifanya ziara katika Hifadhi ya
Msitu wa Lubaga maarufu kama Hashi, iliyopo mkoani Shinyanga, kwa lengo la
kujionea juhudi za uhifadhi wa misitu pamoja na mchango wake katika kulinda
mazingira na kukuza uchumi wa wananchi.
Siku ya Misitu Duniani huadhimishwa kila mwaka tarehe
21 Machi, ikiwa ni jukwaa muhimu la kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa
rasilimali misitu katika maisha ya binadamu na maendeleo ya Uchumi ambapo
Maadhimisho hayo yalianzishwa mwaka 1971 na Food and Agriculture Organization
(FAO), kabla ya kuidhinishwa rasmi na United Nations mwaka 2012 na kuanza
kuadhimishwa kimataifa mwaka 2013.
Kwa upande wa Tanzania, Kanda ya Magharibi
inayojumuisha mikoa ya Katavi, Kigoma, Shinyanga na Tabora ina jumla ya misitu
33 yenye takribani hekta milioni 5.7. Misitu hii kwa kiasi kikubwa ina uoto wa
miombo ambao hupatikana katika nchi chache duniani ikiwemo Mozambique, Zambia, Malawi
na Democratic Republic of the Congo.
Akizungumza kwa niaba ya Kamanda wa TFS Kanda ya
Magharibi, Afisa Misitu Mwandamizi na Mkuu wa Operesheni Kanda hiyo, Shadrack
Msilu alisema uoto huo wa miombo ni muhimu sana kwani unachangia maisha ya
zaidi ya watu milioni 100 katika ukanda huo, huku ukiwa tegemeo kubwa kwa
wananchi wa Tanzania kwa zaidi ya asilimia 87 kutokana na mchango wake
kiuchumi. Hata hivyo, alisema bado misitu inakabiliwa na changamoto za
uharibifu unaotokana na shughuli za kibinadamu.
Kwa mujibu wa takwimu, taifa hupoteza takribani hekta
469,000 za misitu kila mwaka, hali inayohitaji hatua za haraka za uhifadhi na
kwamba katika kukabiliana na hali hiyo, Kanda ya Magharibi imeanza jitihada za
kuongeza misitu kupitia maeneo ya ngitiri, hasa katika Wilaya ya Kishapu,
mkoani Shinyanga.
Kamishna wa Uhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu
Tanzania -TFS, Prof. Dos Santos Silayo alisema Misitu ni mhimili muhimu wa
uchumi wa Tanzania na kwamba kupitia TFS rasilimali hizo zinachangia kwa kiasi
kikubwa maendeleo ya viwanda, hasa vinavyotegemea malighafi za mbao na kwamba sekta
hii hutoa ajira kwa maelfu ya Watanzania kuanzia ngazi ya uzalishaji hadi
usindikaji.
Prof. Dos Santos alieleza kuwa Misitu pia ni chanzo
kikubwa cha mapato ya serikali kupitia ushuru na mauzo ya mazao ya misitu, huku
ikiwezesha biashara za ndani na nje ya nchi. Mbali na hayo, misitu inalinda
mifumo ya ikolojia, ikiwa ni pamoja na vyanzo vya maji na hali ya hewa.
“Umuhimu wa misitu hauishii kwenye uchumi
pekee bali pia unahusiana moja kwa moja na usalama wa taifa ambapo Usalama wa
kiuchumi: Hutoa ajira na kusaidia viwanda, Usalama wa mazingira: Hulinda ardhi,
maji na hali ya hewa”.
“Aidha Usalama wa kijamii: Hupunguza
migogoro ya rasilimali huku Usalama wa kimkakati: Huhifadhi rasilimali muhimu
kwa vizazi vijavyo”.
Mkazi wa Kishapu, Sumai Salum akizungumza kwa niaba ya
wananchi alisema kuwa misitu imekuwa na mchango mkubwa katika maisha yao ya
kila siku, hususan katika kupata kipato kupitia shughuli kama ufugaji nyuki na
uvunaji wa mazao ya misitu.
Sekta ya misitu na nyuki inachangia takribani asilimia
3.3 ya pato la taifa moja kwa moja na hadi asilimia 15 kupitia huduma za
ikolojia, jambo linaloonyesha umuhimu wake mkubwa kiuchumi.
TFS inaendesha programu mbalimbali za maendeleo,
zikiwemo: Uendelezaji wa viwanda vya mazao ya misitu na kuongeza Thamani, Upanuzi
wa mashamba ya miti, Udhibiti wa moto wa misitu na kukabiliana na mabadiliko ya
tabianchi, Elimu kwa umma na ushirikishwaji wa jamii, Matumizi ya teknolojia za
kidijitali kufuatilia rasilimali na Kuendeleza utalii wa ikolojia.
Ufugaji nyuki ni sehemu muhimu ya shughuli za TFS,
hasa katika kukuza uchumi wa vijijini. Tanzania huzalisha zaidi ya tani 30,000
za asali kwa mwaka, huku mikoa ya Tabora, Singida, Katavi na Kigoma ikiwa
vinara wa uzalishaji.
Sekta hiyo hutoa ajira, huongeza kipato cha wananchi
na kusaidia katika uchavushaji wa mazao ambapo tafiti zinaonyesha kuwa nyuki
wanachavusha takribani asilimia 75 ya mimea inayotoa maua na asilimia 35 ya
mazao ya chakula duniani.
Iwapo nyuki watatoweka: Uzalishaji wa chakula
utapungua, Bei za vyakula zitapanda na Mfumo wa ikolojia utadhoofika. Hivyo
basi uhifadhi wa misitu ni sawa na kulinda maisha ya binadamu.
Pamoja na mafanikio yaliyopo, TFS inakabiliwa na
changamoto mbalimbali, zikiwemo: Uvamizi wa misitu na matumizi holela ya ardhi,
Utegemezi mkubwa wa kuni na mkaa kama nishati, Moto wa misituni, Uhaba wa
watumishi, Mabadiliko ya tabianchi, Matumizi madogo ya teknolojia na Miundombinu
isiyoridhisha.
Ili kukabiliana na changamoto hizo, TFS imeweka
mikakati ifuatayo: Kuimarisha mipango bora ya matumizi ya ardhi, Kuongeza doria
na kutumia teknolojia za kisasa kufuatilia misitu, Kuanzisha na kuimarisha
vikosi vya kudhibiti moto, Kuongeza ushirikiano kati ya sekta ya umma na
binafsi, Kutoa mafunzo kwa watumishi na jamii na Kushirikiana na vyombo vya
habari kutoa elimu ya uhifadhi.
Kwa ujumla, Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS)
ni mhimili muhimu katika kulinda rasilimali za taifa na kuchochea maendeleo
endelevu na kwamba kupitia usimamizi madhubuti wa misitu na nyuki, taasisi hii
inaendelea kuhakikisha kuwa rasilimali hizi zinawanufaisha Watanzania wa leo na
vizazi vijavyo.
Ujumbe muhimu unabaki kuwa:
“Kama misitu ni makazi ya nyuki, basi usalama wetu unaanzia msituni.”
SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254

Post a Comment