" VIJANA KUTOKA VYUO VYA SHINYANGA WAPATIWA MAFUNZO YA ITIKADI, WAHIMIZWA KUWA MABALOZI WAZURI WA TAIFA

VIJANA KUTOKA VYUO VYA SHINYANGA WAPATIWA MAFUNZO YA ITIKADI, WAHIMIZWA KUWA MABALOZI WAZURI WA TAIFA

Na Mapuli Kitina Misalaba

Viongozi wa Seneti, matawi pamoja na Serikali za Wanafunzi kutoka vyuo mbalimbali mkoani Shinyanga wamepatiwa mafunzo ya itikadi yaliyolenga kuwajengea uelewa wa kisiasa, uzalendo na uongozi bora.

Mafunzo hayo yamewakutanisha wanafunzi kutoka vyuo mbalimbali ikiwemo Hombolo, St. Joseph na Chuo cha Ualimu Shinyanga (SHYCOM), yakiratibiwa na Seneti ya Vyuo na Vyuo Vikuu Mkoa wa Shinyanga.

Akitoa mafunzo hayo, Katibu wa UVCCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, Naibu Katalambula, ameeleza kwa kina historia ya kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi, akibainisha kuwa chama hicho kilianzishwa rasmi Februari 5, 1977 kufuatia muunganiko wa Tanganyika African National Union na Afro-Shirazi Party.

Amefafanua kuwa vyama hivyo viliongoza pande mbili za Muungano, ambapo TANU kiliongozwa na Julius Nyerere upande wa Tanganyika, huku ASP kikiongozwa na Abeid Amani Karume upande wa Zanzibar.

Katalambula ameeleza kuwa muunganiko huo ulitokana na Muungano wa Tanganyika na Zanzibar wa mwaka 1964 kwa lengo la kuimarisha umoja wa kitaifa, mshikamano wa kisiasa na kuendesha nchi chini ya mfumo mmoja wa chama.

Aidha, amewataka vijana hao kuwa mabalozi wazuri wa Tanzania, kuepuka makundi yasiyofaa na kutumia ipasavyo fursa mbalimbali zinazotolewa na serikali ili kujiletea maendeleo binafsi na ya taifa.

Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Vyuo na Vyuo Vikuu Seneti Taifa, Julias Dekason, amesema kujiunga na Seneti kunawasaidia wanafunzi kujifunza masuala ya uongozi, kujenga mitandao na kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo na siasa za nchi.

Naye Mwenyekiti wa Seneti Mkoa wa Shinyanga, Jackson Aloyce Mwizarubi, amesema Seneti imejipanga kuwasaidia vijana kupata mikopo ya elimu ya juu kwa kuanzisha dawati maalum la usaidizi.

Mwaka jana nikiwa nakaimu nafasi ya mwenyekiti wa Seneti kuna vijana ambao waliomba mikopo nikatoa tangazo kwenye makundi ya vijana wa CCM Shinyanga, baadhi yao walinitumia majina nikawasaidia kuomba. Kwa mwaka huu pia tumejipanga kuweka dawati litakaloshughulikia kuwasaidia vijana kuomba mikopo,” amesema Mwizarubi.

Ameongeza kuwa kwa mwaka huu Seneti mkoa itafanya ziara katika vyuo mbalimbali, kuandaa kongamano la vijana wasomi pamoja na mahafali ya vijana wa Seneti, huku ikiendelea kusaidia vijana wenye uhitaji wa mikopo.

Seneti ya Vyuo na Vyuo Vikuu ni tawi la vijana la UVCCM linalojumuisha wanafunzi na wahadhiri wanaounga mkono chama hicho, likiwa na jukumu la kukuza uzalendo, kusimamia maslahi ya vijana na kutetea sera za serikali.

Katibu Hamasa wa Seneti Mkoa wa Shinyanaga, Sharon Callist Mathias amesema miongoni mwa majukumu ya viongozi wa Seneti ni pamoja na kuhamasisha utekelezaji wa ilani ya uchaguzi, kuandaa viongozi vijana, kuimarisha uzalendo, kushirikiana na vyama vya wanafunzi pamoja na kutoa elimu ya uraia na uongozi kupitia semina na mikutano mbalimbali.

Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo wameushukuru uongozi wa Seneti Mkoa wa Shinyanga kwa kuandaa mafunzo hayo wakieleza kuwa yamewasaidia kuongeza uelewa wa masuala ya uongozi, itikadi na uzalendo, huku wakiahidi kuyatumia maarifa hayo katika kujenga taifa.

Katibu wa UVCCM wilaya ya Shinyanga Mjini, Naibu Katalambula akitoa mafunzo ya itikadi kwa viongozi wa seneti na wanafunzi leo Machi 22, 2026.
Mwenyekiti wa seneti mkoa wa Shinyanga, Jackson Aloyce Mwizarubi akizungumza kuhusu mipango ya seneti na mikakati ya kuwasaidia vijana.



Wanafunzi kutoka vyuo mbalimbali Shinyanga wakishiriki mafunzo ya itikadi yaliyoandaliwa na seneti.

 SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA

 
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA

  • Wasiliana nasi:
    📍 East African Spirits (T) Ltd
    📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254

Post a Comment

Previous Post Next Post