" MHE. BATENGA AWAJENGA KIUCHUMI WANANCHI CHUNYA, ATAJA TAKA KUWA MTAJI MPYA WA MAENDELEO

MHE. BATENGA AWAJENGA KIUCHUMI WANANCHI CHUNYA, ATAJA TAKA KUWA MTAJI MPYA WA MAENDELEO

 

Na Lydia Lugakila-Misalaba  

Mbeya 

Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Mhe. Mbaraka Alhaj Batenga, amewataka wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chunya kuona taka kama fursa muhimu ya kujipatia kipato, akibainisha kuwa taka mbalimbali zinazopatikana katika maeneo tofauti zikichakatwa zina uwezo wa kuzalisha bidhaa mbalimbali zikiwemo nguo, mbolea na bidhaa nyingine nyingi za kiuchumi.


Kauli hiyo ameitoa Aprili 25, 2026 wakati wa zoezi la usafi wa mazingira katika Soko la Uhindini, ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kiwilaya yaliyofanyika katika soko hilo.


“Ndugu zangu wananchi, taka hizi tunazokusanya ni fursa na ni biashara endapo tutajua kuzitenganisha vizuri kwa kuzingatia aina zake. Taka hizi zikichakatwa zinaweza kuzalisha bidhaa nyingi zikiwemo chupa za maji, nguo, mbolea na vitu vingine. Tuitumie vizuri fursa hii kwani mtu anaweza kukusanya taka na kuziuza au kuzichakata kwa matumizi mengine ya kiuchumi,” amesema Mhe. Batenga.


Aidha, ametoa wito kwa wananchi wa Chunya kuendelea kudumisha amani, upendo na mshikamano kama nguzo muhimu za kuendeleza na kuenzi Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.


Vile vile, amesisitiza umuhimu wa kuzingatia usafi wa mazingira katika maeneo ya biashara, taasisi na makazi, akibainisha kuwa usafi ni sehemu ya maisha ya kila siku na ni jukumu la kila mwananchi. Ameongeza kuwa kufanya usafi mara kwa mara kutasaidia kujikinga na magonjwa ya mlipuko.


Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chunya, Dkt. Lucas Theodory, amewataka wananchi kuendelea kuuenzi Muungano kwa vitendo, hususan kwa kudumisha usafi wa mazingira, akisisitiza kuwa afya bora hujengwa na mazingira safi.


Akizungumza kwa niaba ya wananchi waliohudhuria zoezi hilo la usafi, Ndugu Hanifa Hamis na Grace Swila wamesema kuwa pamoja na kuadhimisha siku ya Muungano kwa kufanya usafi, kila mwananchi ana jukumu la kuendelea kufanya usafi kila siku bila kusubiri matukio maalum, kwani shughuli za kila siku ndizo zinazochangia uchafuzi wa mazingira.

Maadhimisho ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar hufanyika kila mwaka tarehe 26 Aprili kama kumbukumbu ya siku hiyo muhimu kwa taifa. Kwa Wilaya ya Chunya, maadhimisho hayo yameanza Aprili 25, 2026 kwa zoezi la usafi wa mazingira.




Post a Comment

Previous Post Next Post