" DC MPWAPWA AWATAKA VIJANA KULINDA AMANI NA KUCHANGAMKIA FURSA

DC MPWAPWA AWATAKA VIJANA KULINDA AMANI NA KUCHANGAMKIA FURSA

 

Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa, Dkt. Sophia Mfaume, amewataka vijana kuendelea kulinda na kutunza amani ya Taifa huku wakichangamkia fursa mbalimbali za kujikwamua kiuchumi.
Amesema hayo katika Kongamano la Uzinduzi wa Jukwaa la Vijana (Youth Platform) lililofanyika katika Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa.

Wito huu unaenda sambamba na nyayo za Jaji Mkuu Mstaafu, Mohamed Chande Othman, ambaye aliwahi kuonya kuwa ukosefu wa ajira na fursa za kiuchumi kwa vijana ni moja ya vyanzo vikuu vinavyoweza kuchochea machafuko na vurugu katika jamii. Hivyo, vijana wametakiwa kulinda amani hiyo kwa utendaji kazi na kutumia vizuri fursa zinazojitokeza ili kujiletea maendeleo badala ya kushawishiwa kuingia kwenye migogoro.
Katika kongamano hilo, Dkt. Mfaume ameishukuru Serikali kwa kuanzisha Wizara ya Maendeleo ya Vijana na kupongeza juhudi za wizara hiyo katika kuandaa mpango wa kuwakutanisha vijana ili kutoa changamoto zao na kushirikishana fursa mbalimbali za maendeleo. Hatua hii inatajwa kuwa nguzo muhimu katika kuwawezesha vijana kiuchumi na kijamii, jambo ambalo ni kinga tosha dhidi ya viashiria vya uvunjifu wa amani.

Kwa upande mwingine, Christian Kapere kutoka Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana, amewakumbusha vijana kuwa kwa sasa Wizara imeandaa dodoso la uundaji wa Baraza la Vijana. Amewaomba vijana kujitokeza na kutoa maoni yao kwa wingi katika dodoso hilo ili kusaidia kuboresha muundo na uendeshaji wa baraza hilo, ambalo litakuwa jukwaa rasmi la kupazia sauti zao.
Naye Omary Punzi, Mratibu wa Makongamano ya Vijana ya kueneza Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Vijana ya mwaka 2007 (toleo la 2024), kupitia Kamati ya Vijana Wazalendo chini ya Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana, amewataka vijana kuitambua Sera hiyo kama mwongozo muhimu wa maendeleo yao. Amesisitiza kuwa uelewa wa sera hiyo utawasaidia kuongeza ushiriki wao wa kimkakati katika shughuli za kijamii na kiuchumi nchini.

Post a Comment

Previous Post Next Post