" MAADHIMISHO YA WIKI YA MAZIWA 2026 KUFANYIKA IRINGA

MAADHIMISHO YA WIKI YA MAZIWA 2026 KUFANYIKA IRINGA

 


Mkoa wa Iringa umepewa heshima ya kuwa mwenyeji wa maadhimisho ya 29 ya Wiki ya Maziwa nchini yanayofanyika kuanzia Mei 25 hadi Juni 1, 2026 katika Viwanja vya Mwembetogwa mjini Iringa, huku wananchi wakihimizwa kuongeza matumizi ya maziwa bora na salama kwa ajili ya afya na maendeleo ya uchumi.

Maadhimisho hayo yaliyoandaliwa na Bodi ya Maziwa Tanzania chini ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi, yanawakutanisha wafugaji, wachakataji wa maziwa, wawekezaji, taasisi za kifedha pamoja na wadau mbalimbali wa tasnia ya maziwa kutoka ndani na nje ya mkoa wa Iringa.

Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maadhimisho hayo, Mkuu wa Mkoa wa Iringa Kheri James amesema sekta ya maziwa imeendelea kuwa mhimili muhimu wa uchumi wa wananchi kwa kutoa ajira, kuboresha lishe na kuongeza kipato kwa maelfu ya familia zinazojishughulisha na ufugaji wa ng’ombe wa maziwa.

Amesema Iringa ni miongoni mwa mikoa inayofanya vizuri katika uzalishaji na ukusanyaji wa maziwa kutokana na mazingira mazuri ya ufugaji pamoja na uwekezaji unaoendelea kupitia Mradi wa Mageuzi ya Tasnia ya Maziwa na Mabadiliko ya Tabianchi (C-SDTP).

“Tunawahimiza wananchi kutumia fursa zilizopo katika tasnia ya maziwa kwa kuongeza uzalishaji, usindikaji na matumizi ya maziwa bora na salama ili kuongeza kipato cha kaya na kuchangia uchumi wa taifa,” amesema.

Kauli mbiu ya mwaka huu inayosema “Rasimisha Biashara ya Maziwa, Okoa Maisha ya Walaji, Ongeza Kipato, Changia Uchumi” inalenga kuhamasisha wafugaji, wasafirishaji na wauzaji wa maziwa kufanya biashara katika mfumo rasmi unaotambulika kisheria huku wakizingatia ubora na usalama wa bidhaa hiyo muhimu ya lishe.

Kwa mujibu wa takwimu za hivi karibuni za Bodi ya Maziwa Tanzania, uzalishaji wa maziwa nchini umefikia zaidi ya lita bilioni 4 kwa mwaka, huku matumizi ya maziwa kwa mtu mmoja mmoja yakiongezeka hadi wastani wa lita 70 kwa mwaka.

Hata hivyo, kiwango hicho bado kiko chini ya mapendekezo ya kimataifa yanayohimiza matumizi ya wastani wa zaidi ya lita 200 za maziwa kwa kila mtu kwa mwaka ili kuchangia lishe bora na afya imara.

Afisa Masoko wa Bodi ya Maziwa Tanzania, Joseph Semu amesema maadhimisho hayo yanalenga pia kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu umuhimu wa kunywa maziwa salama na yenye ubora pamoja na kuhamasisha uwekezaji katika sekta hiyo.

“Tunataka kuona biashara ya maziwa inakuwa rasmi zaidi, wananchi wanapata maziwa salama na wafugaji wanaongeza kipato kupitia sekta hii ambayo inaendelea kukua kwa kasi nchini,” amesema Semu.

Katika kipindi chote cha maadhimisho hayo, shughuli mbalimbali zinaendelea kufanyika katika viwanja vya Mwembetogwa ikiwemo maonesho ya bidhaa na huduma za maziwa, usajili wa wadau wa tasnia hiyo, mafunzo ya ufugaji bora, usindikaji wa maziwa, elimu ya lishe pamoja na kampeni za kuhamasisha unywaji wa maziwa mashuleni na katika vituo vya watoto wenye mahitaji maalum.

Aidha, wadau mbalimbali wanatarajiwa kushiriki kongamano maalum la sekta ya maziwa litakalowakutanisha wafugaji, wachakataji, wawekezaji na wataalamu wa mifugo kujadili namna ya kuimarisha uzalishaji, masoko na usalama wa maziwa nchini.


Mkuu wa mkoa amesema sekta ya maziwa nchini inaendelea kuwa chanzo muhimu cha ajira na mapato kwa mamilioni ya Watanzania, huku Serikali na wadau wake ikiendelea kuwekeza katika kuboresha mifumo ya uzalishaji, ukusanyaji na usindikaji wa maziwa ili kuongeza thamani ya bidhaa hiyo na kupunguza utegemezi wa maziwa kutoka nje ya nchi.

Post a Comment

Previous Post Next Post