" MANKILIGO: MICHEZO NI AJIRA NA CHANZO CHA MAHUSIANO, MANKILIGO AIPONGEZA NIACHEKONA CUP

MANKILIGO: MICHEZO NI AJIRA NA CHANZO CHA MAHUSIANO, MANKILIGO AIPONGEZA NIACHEKONA CUP

Na Mapuli Kitina Misalaba

Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Shinyanga Said Mankiligo ameendelea kumpongeza mwandaaji wa mashindano ya NIACHEKONA CUP 2026 Bwana Paul Daud Augustino kwa juhudi anazoendelea kuzifanya katika kuinua vipaji vya vijana kupitia michezo.

Akizungumza leo Mei 23, 2026 katika muendelezo wa mashindano hayo yanayoendelea kwenye uwanja wa Mwabenda kata ya Solwa, Mankiligo amesema ligi hiyo imekuwa na mchango mkubwa katika kuwaunganisha vijana pamoja na kujenga mahusiano mema ndani ya jamii.

“Naendelea kumpongeza mwandaaji wa mashindano haya kwa kazi kubwa anayofanya. Mashindano haya yanajenga undugu, yanaleta mahusiano lakini pia ni ajira kwa vijana wetu,” amesema Mankiligo.

Aidha amewahimiza waamuzi wanaochezesha mashindano hayo kuhakikisha wanatekeleza sheria 17 za mchezo wa mpira wa miguu kwa usahihi ili kuendelea kudumisha haki, amani pamoja na ushindani wa kweli ndani ya mashindano hayo.

Katika mchezo wa leo, timu ya SHILABELA imeibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya LYABUKANDE FC mchezo ambao umekuwa na ushindani mkubwa huku mashabiki wakifurahia burudani ya soka katika uwanja wa Mwabenda.

Baada ya mchezo huo, Katibu wa Kamati ya Mashindano Sambayi Jilya ametangaza ratiba ya mchezo wa kesho ambapo timu ya KIMANDAGULI itamenyana na KASHISHI katika mchezo unaotarajiwa kuwa na ushindani mkubwa ndani ya NIACHEKONA CUP 2026.

Mashindano hayo yameandaliwa na Bwana Paul Daud Augustino kupitia ufadhili wa Lushu Foundation kwa lengo la kuibua vipaji vya vijana, kuimarisha mshikamano wa jamii pamoja na kukuza michezo katika Mkoa wa Shinyanga.

Kwa huduma za ushereheshaji wa shughuli mbalimbali, matangazo pamoja na burudani unaweza kuwasiliana na MC NIACHEKONA kupitia namba 0757 267 738.


 

Post a Comment

Previous Post Next Post