
📍Ruvuma
Uanzishwaji wa masoko rasmi ya madini pamoja na matumizi ya mfumo wa bei elekezi mkoani Ruvuma, umetajwa kupunguza kwa kiasi kikubwa vitendo vya utoroshaji wa madini huku ukiongeza mapato ya Serikali na kuwanufaisha wachimbaji wadogo.
Mkoa wa Ruvuma kwa sasa una masoko rasmi ya madini mawili likiwemo Soko la Dhahabu na Vito la Songea Mjini pamoja na Soko la Dhahabu na Vito Tunduru, lililozinduliwa rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan Septemba 26, 2024.
Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Ruvuma, Mhandisi Alphonce Bikulamchi, amesema mafanikio hayo yametokana na maboresho yaliyofanywa na Serikali katika usimamizi wa biashara ya madini kupitia masoko rasmi yenye uwazi na ushindani wa kibiashara.
Amesema kabla ya kuanzishwa kwa masoko hayo, baadhi ya wachimbaji walikosa maeneo rasmi ya kuuza madini yao hali iliyochochea biashara holela na utoroshaji wa madini, jambo lililoikosesha Serikali mapato na kuwafanya wachimbaji wadogo kuuza madini yao kwa bei isiyo na tija.
“Kwa sasa wachimbaji wanapata taarifa sahihi za bei elekezi za madini yao, jambo ambalo limeongeza uwazi, kuondoa mianya ya udanganyifu na kuongeza imani katika biashara ya madini,” amesema Mhandisi Bikulamchi.
Ameeleza kuwa uwepo wa wanunuzi kutoka ndani na nje ya nchi katika masoko hayo umeongeza ushindani wa bei na kuwawezesha wachimbaji kuuza madini yao kwa thamani inayostahili.
Aidha, amesema Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya biashara ya madini kwa kuimarisha usimamizi wa masoko na kutoa elimu kwa wachimbaji ili kuhakikisha sekta hiyo inaendelea kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa pamoja na maendeleo ya wananchi.
Kwa mujibu wa Mhandisi Bikulamchi, hatua hiyo pia imeongeza ushiriki wa wachimbaji wadogo katika uchumi rasmi na kusaidia kudhibiti vitendo vya utoroshaji wa madini mkoani Ruvuma.

SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254
Post a Comment