Na Edington Mukiza Ezron, Misalaba Media
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU)
Mkoa wa Shinyanga imefanikiwa kuokoa jumla ya shilingi 21,897,954 kupitia
shughuli mbalimbali za ufuatiliaji wa matumizi ya fedha za umma, uchunguzi wa
tuhuma za rushwa pamoja na uelimishaji wa wananchi katika kipindi cha Januari
hadi Machi 2026.
Hayo yameelezwa leo Mei 29, 2026 na Mkuu wa TAKUKURU
Mkoa wa Shinyanga, Donasian Kessy, wakati akizungumza na waandishi wa habari
kuhusu taarifa ya utekelezaji wa shughuli za taasisi hiyo kwa robo ya tatu ya
mwaka.
Kessy amesema kati ya fedha hizo, shilingi 5,540,254
zimeokolewa kupitia ufuatiliaji wa mradi wa ujenzi wa shule mpya ya awali na
msingi ya Tinde “B” katika Manispaa ya Shinyanga, baada ya kubainika kuwa kiasi
cha shilingi 5,316,304 kilipaswa kulipwa katika Mamlaka ya Mapato Tanzania
(TRA) kama kodi ya zuio, huku shilingi 223,950 zikiwa ushuru uliopaswa kulipwa
katika Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga.
Ameongeza kuwa shilingi 9,672,000 zimepatikana kupitia
elimu ya uadilifu iliyotolewa kwa viongozi wa Vyama vya Msingi vya Ushirika wa
Kilimo na Masoko (AMCOS) wilayani Kishapu, ambavyo vilikuwa vinadai fedha
kutoka kwa makampuni ya ununuzi wa zao la pamba. Amesema elimu hiyo imechangia
kurejeshwa kwa fedha hizo kutoka katika makampuni matatu yaliyokuwa yanadaiwa.
Pia amesema TAKUKURU imefanya ufuatiliaji wa matumizi
ya fedha katika utekelezaji wa miradi 19 ya maendeleo yenye thamani ya shilingi
3,906,564,882 katika sekta za elimu, afya, maji na miundombinu.
Aidha, kupitia uchunguzi wa tuhuma mbalimbali za
ubadhirifu wa mali za umma pamoja na hatua za kisheria zilizochukuliwa dhidi ya
watuhumiwa, shilingi 6,685,700 zimerejeshwa serikalini baada ya baadhi ya
watuhumiwa kufikishwa mahakamani na kukiri makosa yao.
Kessy amesema katika kipindi hicho taasisi hiyo
ilipokea jumla ya malalamiko 89, ambapo malalamiko 55 yalihusu rushwa na 34
hayakuhusu rushwa. Ameeleza kuwa uchunguzi wa malalamiko yanayohusu rushwa
unaendelea katika hatua mbalimbali, huku yale yasiyohusu rushwa yakipelekwa
katika mamlaka husika kwa hatua zaidi.
Hata hivyo, amezitaka taasisi zote za umma kuendelea kutoa huduma kwa wananchi kwa kuzingatia maadili na uwajibikaji, huku akiwaomba wananchi wa Mkoa wa Shinyanga kushirikiana na TAKUKURU katika juhudi za kuzuia na kupambana na rushwa, hasa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo na utoaji wa huduma za kijamii.

Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga, Donasian Kessy.

SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254




Post a Comment