" TAKWIMU ZA MIGOGORO ZAFICHULIWA SHINYANGA, SAMIA LEGAL AID YAWAFIKIA WANANCHI 142,532 KWA SIKU CHACHE

TAKWIMU ZA MIGOGORO ZAFICHULIWA SHINYANGA, SAMIA LEGAL AID YAWAFIKIA WANANCHI 142,532 KWA SIKU CHACHE

Wananchi wa Mkoa wa Shinyanga wameendelea kunufaika na kampeni ya msaada wa kisheria inayotekelezwa katika halmashauri mbalimbali za mkoa huo kupitia mpango wa Samia Legal Aid, wenye lengo la kusaidia wananchi kutatua changamoto za kisheria zinazowakabili katika jamii.

Akizungumza na Misalaba Media Mei 14, 2026, Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma ya Msaada wa Kisheria Mkoa wa Shinyanga ambaye pia ni Mkurugenzi wa shirika la PACESHI, Bwana John Shija, amesema kampeni hiyo imeendelea kupokelewa vizuri na wananchi huku ikipeleka huduma katika maeneo mbalimbali ili kuwafikia wananchi wengi zaidi.

Shija amesema lengo kuu la kampeni hiyo ni kutoa elimu ya sheria pamoja na kusaidia wananchi kutatua migogoro mbalimbali ikiwemo ya mirathi, ardhi, ndoa na ukatili wa kijinsia ambayo imekuwa ikisababisha migogoro ndani ya jamii.

Ameeleza kuwa baadhi ya wananchi wamekuwa wakipoteza mali au haki zao kutokana na kutofuata taratibu sahihi za kisheria, hasa katika masuala ya mirathi ambapo wengine huuza mali za marehemu bila kushirikisha wahusika halali au kupata vibali vinavyotakiwa kisheria.

“Katika masuala ya mirathi, tunasisitiza wananchi kufuata utaratibu wa kisheria ili kulinda haki za kila mmoja na kuondoa migogoro isiyo ya lazima ndani ya familia,” amesema Shija.

Aidha amesema kampeni hiyo pia inalenga kutoa elimu kuhusu haki za wanawake na watoto, akibainisha kuwa bado baadhi ya wanawake wanakosa haki zao katika mirathi kutokana na ukosefu wa elimu ya sheria na mila kandamizi.

Ameongeza kuwa wanawake wanashauriwa kuhakikisha ndoa zao zinasajiliwa kisheria ili kulinda haki zao na za watoto endapo kutatokea migogoro ya kifamilia au mgawanyo wa mali.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa kupitia kampeni hiyo, wananchi 142,532 tayari wamefikiwa na huduma mbalimbali za msaada wa kisheria kwa kipindi kifupi tangu kuanza kwa kampeni Mei 6, 2026, huku wanaume wakiongoza kwa kujitokeza kupata huduma hizo.

Takwimu hizo pia zinaonyesha kuwa jumla ya migogoro 2,051 imepokelewa, huku migogoro 1,803 ikiwa imefanikiwa kupatiwa ufumbuzi kupitia ushauri wa kisheria na njia mbalimbali za usuluhishi.

Shija amesema huduma hizo zinatolewa bure kwa wananchi wote bila ubaguzi, huku akiwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kabla ya kampeni hiyo kuhitimishwa Mei 20, 2026.

Amesema kampeni hiyo inayoratibiwa na Wizara ya Katiba na Sheria imeendelea kuwa msaada mkubwa kwa wananchi katika kuelewa haki zao na kupata suluhisho la changamoto za kisheria kwa njia ya amani na sheria.

SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA

🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA

  • Wasiliana nasi:
    📍 East African Spirits (T) Ltd
    📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254

Post a Comment

Previous Post Next Post