" VITENDO VYA RUSHWA VYATAJWA KUDUMAZA MAENDELEO YA JAMII NCHINI

VITENDO VYA RUSHWA VYATAJWA KUDUMAZA MAENDELEO YA JAMII NCHINI

 Na Edington Mukiza Ezron, Misalaba Media

Baadhi ya wananchi katika Manispaa ya Shinyanga wamewataka viongozi wa serikali pamoja na watumishi wa taasisi mbalimbali kuwa waadilifu na kuacha kujihusisha na vitendo vya rushwa ili kulinda haki za wananchi na kuchochea maendeleo ya jamii.

Wakizungumza na Misalaba Media kwa nyakati tofauti Mei 8, 2026, wananchi hao wamesema vitendo vya rushwa vinaendelea kuathiri utoaji wa huduma katika taasisi mbalimbali na kusababisha wananchi wengi kukosa haki zao za msingi.

Mmoja wa wananchi hao, William Muhangwa, amesema baadhi ya viongozi na watumishi wa taasisi za umma wamekuwa wakijihusisha na vitendo vya rushwa vinavyowakosesha wananchi wasiokuwa na uwezo kupata huduma kwa haki na kwa wakati.

Ameongeza kuwa baadhi ya wananchi hulazimika kutoa rushwa ili kuharakisha huduma kutokana na ucheleweshaji unaofanywa katika baadhi ya ofisi na taasisi.

Aidha, wananchi hao wameeleza kuwa ukosefu wa ajira nao umechangia kuongezeka kwa vitendo vya rushwa, kutokana na uwepo wa wahudumu wachache wanaotoa huduma kwa idadi kubwa ya wananchi, hali inayosababisha mlundikano wa wahitaji wa huduma.

Pia wamebainisha kuwa rushwa inazorotesha maendeleo ya jamii kwa kuathiri utekelezaji wa miradi ya maendeleo, huduma za kijamii pamoja na haki za binadamu, hivyo jamii inapaswa kushirikiana kupinga vitendo hivyo kwa manufaa ya taifa.

Wameongeza kuwa waajiri wanapaswa kuwasisitiza watumishi wa taasisi mbalimbali kuzingatia maadili ya kazi na kuacha kupokea rushwa ili kulinda haki za wananchi pamoja na heshima ya taasisi zao.

Hata hivyo, wananchi hao wameitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kuendelea kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya watakaobainika kujihusisha na vitendo vya rushwa, sambamba na kuongeza elimu kwa jamii kuhusu madhara ya rushwa na umuhimu wa kupambana nayo.

SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA

🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA

  • Wasiliana nasi:
    📍 East African Spirits (T) Ltd
    📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254

 

Post a Comment

Previous Post Next Post