" DUARA FC YATINGA NUSU FAINALI BAADA YA KUIFUNGA MAWEMIRU FC, MWENYEKITI WA SOKA SHINYANGA AZITAKA TIMU ZA MKOA NA DARAJA LA KWANZA KUSAKA VIPAJI NIACHEKONA CUP

DUARA FC YATINGA NUSU FAINALI BAADA YA KUIFUNGA MAWEMIRU FC, MWENYEKITI WA SOKA SHINYANGA AZITAKA TIMU ZA MKOA NA DARAJA LA KWANZA KUSAKA VIPAJI NIACHEKONA CUP


Na Mapuli Kitina Misalaba

Timu ya Duara FC imefanikiwa kutinga hatua ya nusu fainali ya mashindano ya NIACHEKONA CUP 2026 baada ya kuibuka na ushindi wa goli 1-0 dhidi ya Mawemiru FC katika mchezo wa robo fainali uliochezwa leo Juni 14, 2026 katika Uwanja wa Mwabenda, Kata ya Solwa.

Bao pekee la ushindi kwa Duara FC lilifungwa na Neno Michael katika kipindi cha kwanza cha mchezo huo, bao ambalo lilidumu hadi dakika 90 na kuipa timu yake tiketi ya kusonga mbele katika hatua inayofuata ya mashindano hayo.

Mchezo huo uliokuwa na ushindani mkubwa uliwashuhudia wachezaji wa Mawemiru FC wakifanya juhudi za kutafuta bao la kusawazisha, lakini walishindwa kuvunja ngome ya Duara FC iliyokuwa imara hadi mwisho wa mchezo.

Kwa matokeo hayo, safari ya Mawemiru FC imehitimishwa katika hatua ya robo fainali, huku Duara FC ikijiweka katika nafasi nzuri ya kuwania ubingwa wa mwaka huu.

Baada ya ushindi huo, nahodha pamoja na kocha wa Duara FC wametuma ujumbe kwa wapinzani wao wa hatua ya nusu fainali, Ufukunyungu FC, wakisema kuwa timu yao ipo tayari kwa pambano hilo na wana imani kubwa ya kupata ushindi utakaowapeleka moja kwa moja katika hatua ya fainali.

Kwa mujibu wa ratiba ya mashindano hayo, nusu fainali ya kwanza itawakutanisha Ufukunyungu FC dhidi ya Duara FC katika mchezo unaotarajiwa kuwa na ushindani mkubwa kutokana na kiwango walichoonyesha timu hizo katika hatua zilizopita.

Akizungumza baada ya mchezo huo, Katibu wa Kamati ya Mashindano ya NIACHEKONA CUP, Sambayi Jilya, ametangaza ratiba ya mchezo wa kesho ambapo Nyandolwa FC kutoka Kata ya Mwenge Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga itamenyana na Bulige FC kutoka Halmashauri ya Msalala Wilaya ya Kahama katika mchezo mwingine wa robo fainali.

Sambayi Jilya amewahimiza wananchi na wadau wa michezo kuendelea kujitokeza kwa wingi katika Uwanja wa Mwabenda kushuhudia michezo iliyobaki ya mashindano hayo.

Mgeni maalum wa mchezo wa leo alikuwa Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Shinyanga, Said Mankiligo, ambaye aliambatana na baadhi ya wachezaji wa zamani waliowahi kuandika historia ya soka katika Kijiji cha Mwabenda.

Mankiligo amempongeza mwandaaji wa NIACHEKONA CUP 2026, Paul Daud Augustino maarufu MC NIACHEKONA, kwa kuendelea kuibua vipaji vya vijana kupitia michezo.

Aidha, amezihimiza timu zinazoshiriki Ligi Daraja la Kwanza, Ligi ya Mabingwa wa Mikoa na mashindano mengine makubwa kujitokeza kufuatilia michezo ya NIACHEKONA CUP ili kupata fursa ya kusajili wachezaji wenye vipaji wanaoshiriki mashindano hayo.

Amesema NIACHEKONA CUP imeendelea kuwa jukwaa muhimu la kuibua vipaji vya vijana na kwamba kuna wachezaji wengi wenye uwezo mkubwa wanaoweza kupata nafasi katika timu mbalimbali kwa gharama nafuu.

Mashindano ya NIACHEKONA CUP 2026 yameandaliwa na Paul Daud Augustino maarufu MC NIACHEKONA kwa ufadhili wa Shirika la Lushu Foundation, yakilenga kuibua vipaji vya vijana, kukuza michezo na kuimarisha mshikamano wa jamii.

Kwa huduma za MC, matangazo na ushereheshaji wa matukio mbalimbali, wasiliana na MC NIACHEKONA kupitia namba 0757 267 738.

Kikosi cha (Manonga) Duara FC.

 

Post a Comment

Previous Post Next Post