" EWURA YAFIKIA WANANCHI,MAONESHO YA WIKI YA UTUMISHI WA UMMA 2026

EWURA YAFIKIA WANANCHI,MAONESHO YA WIKI YA UTUMISHI WA UMMA 2026

Na Mwandishi Wetu
Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imeanza kushiriki katika Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma mwaka 2026 yaliyoanza rasmi leo, tarehe 16 mpaka 23 Juni, yanayofanyika katika Viwanja vya Chinangali Park jijini Dodoma
Akizungumza kuhusu ushiriki wa EWURA katika maonesho hayo, Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala wa EWURA, Bi. Hawa Ramadhan Mniga, amesema maonesho hayo ni fursa muhimu kwa Mamlaka hiyo kuwafikia Watanzania na kuwapatia uelewa kuhusu majukumu yake katika usimamizi wa sekta za nishati na maji.
“Wananchi watakaotembelea banda la EWURA watapata fursa ya kujifunza masuala mbalimbali ikiwemo mifumo mbalimbali ya kidijitali inayotumiwa na Mamlaka katika utoaji wa huduma kwa wateja, pamoja na maboresho yanayoendelea kufanyika kwa lengo la kuongeza ufanisi, kasi na ubora wa utoaji wa huduma,” amesema Bi. Mniga.
Ameongeza kuwa eneo lingine lililopatiwa kipaumbele ni uhamasishaji wa matumizi ya nishati safi ya kupikia, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kufanikisha lengo la Taifa la kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.
Aidha, ametoa rai kwa wananchi, wadau wa sekta mbalimbali na washiriki wa maonesho hayo kutembelea banda la EWURA ili kupata elimu, kuuliza maswali na kufahamu kwa undani huduma zinazotolewa na Mamlaka hiyo.

Post a Comment

Previous Post Next Post