" MACHINGA WA KINONDONI WAJITENGA NA MAANDAMANO, WASISITIZA KULINDA AMANI

MACHINGA WA KINONDONI WAJITENGA NA MAANDAMANO, WASISITIZA KULINDA AMANI

 


Wafanyabiashara wadogo maarufu kama machinga katika Wilaya ya Kinondoni Jijini Dar Es Salaam leo Juni 15, 2026 wamemuahidi Rais Samia Suluhu Hassan kuwa hawatashiriki maandamano ya Julai 07, 2026, wakiweka wazi msimamo wao dhidi ya harakati hizo zinazosukumwa na wanaharakati kutoka nje ya nchi kupitia mitandao ya kijamii.

Wafanyabiashara hao akiwemo Makamu Mwenyekiti wa Machinga wa Wilaya ya Kinondoni Bi. Palejia Michael Mushi, wamesema wao wameamua kuchagua na kulinda amani ya nchi na usalama wa mali zao, hivyo hawatakuwa sehemu ya maaandamano hayo kutokana na historia ya kile kilichotokea Oktoba 29, 2026 pale yalipofanyika matukio ya ghasia na uvunjifu wa amani kwa kisingizio cha maandamano.

"Tupo hapa kuendelea kuwahamasisha machinga wa Kinondoni na Tanzania kwa ujumla kwamba maandamano haya yanayohamasishwa na watu ambao hata hawapo hapa Nchini, yatatuathiri sisi na biashara zetu. Niwasihi Machinga wote na Vijana kwa ujumla tusikubali kuingia katika ushawishi huo wa kuandamana kwa maslahi ya watu wachache wakituangalia tukiangamia. Mama yetu Samia amekubali kuwa mlezi wetu machinga na kutokana na hilo nami nitumie fursa hii kumuahidi kuwa tutakuwa walinzi wa amani na hatutakubali amani hii inayotupa fursa ya kuendelea na mambo yetu kuweza kuharibiwa." Amesema Bi. Mushi.

Katika hatua nyingine kundi hilo la machinga limehimiza matumizi ya majadiliano kama njia pekee salama ya kutatua changamoto zilizopo Nchini, wakiishukuru pia serikali ya Rais Samia kwa kuendelea kuwa karibu na makundi mbalimbali ya Kijamii ikiwemo wafanyabiashara hao wadogo, kwani wamekuwa wakisikilizwa kila wakati wanapopitia changamoto za kibiashara.

Aidha, wafanyabiashara hao wadogo wametoa wito kwa machinga wenzao nchi nzima kutokubali kurubuniwa na watu wenye maslahi binafsi. Wamewataka wafanyabiashara wote wawe macho na wasikubali kutumiwa na wachache wanaotafuta umaarufu wa kisiasa au kijamii kwa kuwaponza wanyonge, wakisisitiza kulinda amani ya nchi na kuendelea na biashara zao kama kipaumbele chao kikubwa kwa sasa.

Post a Comment

Previous Post Next Post