Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, amesema kuwa maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika ni kumbusho kwa jamii kuhusu wajibu wa kulinda na kuendeleza haki za watoto, sambamba na kumbukumbu ya watoto wa Soweto nchini Afrika Kusini waliopigania haki ya kupata elimu bora.
Akizungumza Juni 16, 2026 jijini Dodoma, Prof. Mkenda ameeleza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inaendelea kuiweka elimu miongoni mwa vipaumbele vyake, sambamba na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye amesisitiza kuwa kila mtoto wa Kitanzania lazima apate elimu.
Kwa msingi huo, Waziri Mkenda amesema Serikali imeweka mkazo katika kuhakikisha usawa na ujumuishi katika elimu kwa watoto wote, ikiwemo kuimarisha usawa wa kijinsia ili kila mtoto apate fursa ya kujifunza na kufikia ndoto zake.
“Hakuna mtoto atakayeachwa nyuma katika mfumo wa elimu. Hata mabinti waliopata ujauzito wanaruhusiwa na wanapaswa kurejea shuleni kuendelea na masomo yao,” alisisitiza Prof. Mkenda.
Aidha, amebainisha umuhimu wa kuhakikisha shule zinakuwa na mazingira salama na rafiki kwa watoto wote ili kuwawezesha kujifunza kwa ufanisi na kustawi kielimu.
Prof. Mkenda ametoa wito kwa wazazi, walezi, viongozi wa dini, mashirika mbalimbali na wadau wa maendeleo kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha watoto wote wanapata haki zao za msingi, ikiwemo elimu bora, huduma za afya, maji safi na mazingira salama ya kukua na kuendelea.
Post a Comment