" STAKABADHI ZA GHALA KUINUA BIASHARA YA MIFUGO NCHINI

STAKABADHI ZA GHALA KUINUA BIASHARA YA MIFUGO NCHINI

 

Na Mwandishi Wetu

WAFUGAJI nchini wamefurahishwa na mpango wa matumizi ya Mfumo wa Stakabadhi za Ghala kwenye sekta ya mifugo wakidai kuwa utaleta manufaa makubwa katika masoko na biashara shindani ya mifugo.

Akizungumza baada ya kutembelea banda la Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB) katika Maonesho ya Mifugo na Mnada wa Kimataifa yanayofanyika katika Shamba la Mbogo, Chalinze mkoani Pwani, Mwenyekiti wa Chama Cha Wafugaji Tanzania (CCWT), Mrida Mshota, amesema mfumo huo utasaidia kutatua changamoto ya masoko ya mifugo nchini.

Amesema kupitia mpango huo wafugaji watapata fursa ya kujitangaza katika masoko ya kimataifa na kuuza mifugo yao kwa uhakika zaidi.

“Ukiwa na shamba lako na likasajiliwa na serikali sasa unakuwa na uhakika wa kuuza mifugo kwenye masoko makubwa ya kimataifa. Mpango huu ni mzuri na naiomba serikali iweke mkazo mkubwa kuhakikisha unaanza kutekelezwa haraka. Waziri Mkuu tayari alishasema jambo hili lishughulikiwe kwa haraka ili liwe na tija kwa wafugaji,” amesema Mshota.

Aidha, ameishauri Wizara ya Viwanda na Biashara kuweka mikakati madhubuti katika maeneo mbalimbali nchini ili utekelezaji wa mfumo huo uanze kabla ya mwaka huu kuisha.

“Sisi tuna kanda nane, hivyo tukitumia vizuri kanda zote serikali itakwenda kukusanya mapato bila kutumia nguvu kubwa. Kwa sasa utoroshaji wa mifugo ni mkubwa kwani baadhi ya wafugaji wanapeleka mifugo nje ya nchi bila utaratibu rasmi, lakini tukianza kutumia mfumo huu wenye masoko ya uhakika, tatizo hilo litapungua kwa kiasi kikubwa,” amesema.

Naye, Afisa Ubora wa WRRB, Bw. Anatolius Kabyemera, amesema mfumo huo utaleta uwazi katika biashara ya mazao na mifugo, kuongeza ushindani wa bei na kuhakikisha wafugaji pamoja na wakulima wanapata thamani halisi ya bidhaa zao.

Post a Comment

Previous Post Next Post