" WANASIASA WAPAZA SAUTI KUTAKA MARIDHIANO

WANASIASA WAPAZA SAUTI KUTAKA MARIDHIANO

 

Chama cha ACT Wazalendo, chini ya Mwenyekiti wake Othman Masoud Othman (Omo) kimefanya mkutano na wadau wa demokrasia kujadili namna ya kudumisha amani na kupata maridhiano baada ya matukio ya ghasia ya Oktoba 29, 2025 wakati na baada ya uchaguzi.
Katika mkutano huo, Omo alianzisha mjadala kwa kuwasilisha maoni yake lakini mwisho akatoa ushauri kwamba wanapaswa kuchagua njia inayofaa kwa nchi na kwamba viongozi wa kisiasa wanapaswa kuongoza mchakato huo.

Mada hiyo ya Omo, inawainua wadau wa siasa waliohudhuria majadiliano hayo na kutaka uwepo mjadala wa kitaifa ili kufikia maridhiano. 
Katika kuchangia, Katibu Mkuu wa Chama cha Maendeleo ya Umma (CHAUMMA) na mgombea urais katika uchaguzi wa mwaka 2025 Salum Mwalimu, anasema maridhiano yanahitajika na yeyote atakayetaka yaliyotokea Oktoba 29, yajirudie huyo hatokuwa miongoni mwa Watanzania na lazima akataliwe.
“Yeyote mwenye ndoto ya kwamba yale ni mazuri tuendelee kuyazungumza kwa madaha ili yajirudie, huyo hatokuwa miongoni mwetu Watanzania na huyo lazima tumkatae, lazima tuseme hapana tena kujirudia kwa matukio yaliyotokea tarehe 29, tuyazungumze kwa kuponyana tusiyazungumze kwa kuyachochea na kuyafanya kumbukumbu ya kudumu ndani ya nafsi zetu na rekodi ya maisha yetu,” anasema.

Mwalimu, aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Zanzibar, anasisitiza kuwa jambo kubwa ni kutazama namna ya nchi kutoka ilipo kwani kila mmoja kwa wakati wake anajua sababu na kilichotokea siku ya uchaguzi huo, hivyo haina haja ya kukumbushana na badala yake watu wasonge mbele.

“Nasema kweli na Mungu atanisamehe, hatupingani kwamba tulifikaje Oktoba 29, hatupingani kwamba kuna mauaji yalitokea, hatupingani kwamba kuna tatizo kubwa la ajira kwa vijana wenzetu nchi hii, wote tunajua, tunashindana kwenye namna ya kutoka hapa… changamoto kubwa kwa maoni yangu imekuwa ni kushindana maneno kuliko kutoa majawabu, kubadilishana majukwaa na kuoneshana umahiri wa kusema, ukweli ni kwamba tunashindwa kugusa kiini cha vipi tutoke hapa tulipo,” anasema.

Anampongeza Omo na chama chake cha ACT kwa kuitisha mjadala huo na kumtaka kuwa kiongozi kwa upande wa wapinzani katika kuhakikisha maridhiano yanapatikana.

“Umetoa jawabu lisimamie, lisimamie usione aibu, wewe ni mkongwe wetu yeyote atakayetoka kukupinga tutamuuliza unampinga Omo kwa lipi, kama ulivyoandika kwenye kijitabu hiki na nanukuu ‘hatua zote nilizozitaja zinahitaji mwafaka wa kitaifa utakaotupeleka mbele kama taifa, hivyo tunahitaji kuanzisha jukwaa la majadiliano ya kitaifa litakaloongozwa na misingi tuliyoitaja ya ukweli, haki na uwajibikaji ili kukubaliana juu ya namna bora ya kuzifikia hatua hizo’,” anasema Mwalimu akinukuu sehemu ya kitabu kilichoandikwa na Omo.
“Ukiacha hivi tutabakia na mjadala, nenda kaanzishe jukwaa au vyovyote utakavyoliita, na usilibebe kama Mwenyekiti wa chama, beba kama kiongozi mwandamizi wa kisiasa na wote tupo nyuma yako... 
Tunataka upande wa pili wawajibike sisi tunawajibikaje kama viongozi wa kisiasa, tunautaka ukweli tutaupata wapi, tunataka watoke nje (watu watakaoongoza maridhiano) wakija wanapokelewa na nani? wanakaa na nani?, nenda kaanzishe kamati chagua watu kadri unavyoweza chukua uongozi hatuna uongozi kwa upande wetu sisi (wapinzani) nenda katuongoze,” anasema.
Miongoni mwa wadau waliohudhuria majadiliano hayo ni mwandishi na mchambuzi wa masuala ya siasa, Ezekiel Kamwaga ambaye anasema nchi inatakiwa kuwa na utashi wa kisiasa kabla ya kuzungumza ukweli. 

“Viongozi mtuongoze… sasa hivi unaona kama viongozi wako mitandaoni zaidi, kiongozi mzuri ni yule anayekaa mbele wakati wa kuzomewa wakati wa sifa anakaa nyuma, lakini sasa hivi naona kama viongozi wanakaa nyuma hivi… tokeni kwenye hili tulipambanie taifa letu,” anasema Kamwaga.

Kwa upande wa mwanasiasa Odero Odero anawataka baadhi ya viongozi kutafuta Suluhu wakati huu taifa liko kwenye mkwamo badala ya kulia na kutupa lawama. 

“Niwaambie mambo muhimu, Othman (Omo) Rais Samia (Suluhu Hassan) ni dada yako, Zito (Kabwe- kiongozi mstaafu wa ACT) Rais Samia ni mama yako, Heche (John- Makamu Mwenyekiti wa Chadema) Rais Samia ni mama yako mkianza tabia ya kuogopana na kujificha hatutafika, nawashauri mkabilini Rais Samia kwenye meza ya mazungumzo tukitoka hapa ili kieleweke,” anasema.

Suala la maridhiano lipo kwenye falsafa ya 4R ya Rais Samia zikimaanisha Maridhiano, Ustahimilivu, Mageuzi na Kujenga upya. Baada ya kupokea ripoti ya Tume ya Kuchunguza Matukio Wakati na Baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, iliyokuwa chini ya Jaji Othman Chande, Rais Samia alisema ataunda tume ya maridhiano kama ripoti hiyo ilivyoshuuri.

Aidha, katika kuelekea maridhiano, Rais ameunda Tume ya Uchunguzi wa Kijinai, jambo ambalo limewafurahisha wanasiasa wengi, akiwemo Katibu Mkuu wa Chaumma, ambaye anasema tume hiyo ina umuhimu kwa sababu inaendelea na utekelezaji wa mapendekezo ya tume ya Jaji Chande na isipokuwepo mchakato wa maridhiano utachelewa.

“Kumekuwa na kilio kikubwa baada ya ripoti ya tume ya Jaji Chande na kubwa watu wakitaka uwajibikaji, tume ya Jaji Chande isingeweza kuchambua kwa kina, naamini hilo ni jambo kubwa linalotakiwa kuangaliwa katika mazingira ya tahadhari zote ili kuepuka mgogoro mwingine, kuna waliohusika kuandaa vurugu zile, kuumiza watu,” anasema.

Mwingine anayeunga mkono tume hiyo ni aliyekuwa mgombea Urais katika uchaguzi wa mwaka 2025 kupitia chama cha Makini, Costa Kibonde ambaye anaamini tume hiyo itamaliza ‘kiporo’ kilichoachwa na tume ya Jaji Chande.

Post a Comment

Previous Post Next Post