Na, Egidia Vedasto,
Misalaba Media, Arusha.
Mkutano wa tatu wa mafunzo Kwa Mawakili wa serikali yamehitimishwa rasmi ambapo Mawakili wametakiwa kuzingatia mada walizofundishwa kwa maslahi mapana ya Taifa.
Akifunga mafunzo hayo Jijini Arusha Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Zainabu Katimba amewataka Mawakili kutumia Sheria kama nyenzo ya ukuaji wa uchumi na kulinda taifa katika mazingira ya ushindani.
Aidha amewakumbusha kuwa, mafunzo waliyoyapata yawasaidie kuwa wabunifu kuendana na teknolojia ya kisasa, kusimamia mikataba ya uwekezaji na kuleta mageuzi.
"Nashauri Ofisi ya Mwanasheria mkuu kufanya tathmini ya mara kwa mara kuhakikisha mafunzo yanayotolewa yanazingatiwa Kwa kuonyesha uwajibikaji, weledi na maarifa katika utekelezaji wa majukumu yao. Serikali itaendelea kuunga mkono mafunzo hayo muhimu na tayari imetenga sh. Bilioni 6 kuwezesha mafunzo bila kulipia" Amesema Katambi.
Katika namna hiyo hiyo Naibu Mwanasheria Mkuu wa serikali Samwel Maneno ameishukuru serikali Kwa kutenga bajeti ya bilioni 6 kuwezesha mafunzo Kwa Mawakili wa serikali na kuahidi kuwa mafunzo hayo ni muhimu na yanaongeza kasi ya maendeleo kwa taifa.
Sambamba na hayo amewaasa Mawakili kuzingatia mafunzo waliyopewa, kuayatumia kama mbinu wakati wa kutekeleza majukumu yao, kutoa msaada wa kisheria katika jamii, kukabili makosa ya jinai, kusoma mikataba kuielewa na kushauri.
"Natoa wito kwa kila Mkurugenzi wa huduma za sheria kuhakikisha Mawakili wote wanajiorodhesha katika daftari la orodha, Pia tutafuatilia kwa karibu kuhakikisha Sheria ndogo zinatungwa kuendana na Katiba na Sheria mama" amesema.
Kwa upande wake Rais wa chama cha Mawakili nchini Bonaventure Mwambaja amesema yeye na safu yake ya uongozi wamejipanga kuimarisha chama kwa kuzingatia misingi, weledi na kuleta matokeo chanya.
"Naahidi kushirikiana bega kwa bega na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu lengo ni kuona tunafikia lengo la Dira ya taifa 2050 na kuisaidia serikali katika mikataba ya kimataifa" amesema Wakili Mwambaja.



Post a Comment