" ZANZIBAR KULETA MADEREVA WAKE CHUO CHA UFUNDI ARUSHA KUJIFUNZA KOZI YA UDEREVA VIP

ZANZIBAR KULETA MADEREVA WAKE CHUO CHA UFUNDI ARUSHA KUJIFUNZA KOZI YA UDEREVA VIP

Na Seif Mangwangi, Arusha

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar imesema ina mikakati ya kuleta madereva kutoka visiwani humo kuja katika chuo cha ufundi Arusha (ATC), kujifunza ujuzi wa kuendesha magari tofauti ikiwemo ya viongozi na kuepusha ajali zinazotokea mara kwa mara.

Mkufunzi wa mafunzo ya udereva katika chuo cha ufundi Arusha, Gilbert Mollel, akimpa maelezo Naibu Waziri wa ujenzi na uchukuzi kutoka Zanzibar, Badria Masoud aliyevaa kitambaa cha bluu juu ya namna injinia ya gari inavyofanyakazi. Wa kwanza kushoto ni Mkuu wa chuo cha ATC Profesa Mussa Chacha

Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa wizara ya ujenzi na uchukuzi Zanzibar, Badria Atai Masoud, Julai16, 2026 alipofanya ziara katika chuo cha ufundi Arusha na kujionea mitambo mbalimbali inayotumika kufundishia wanafunzi chuoni hapo ikiwemo karakana ya magari.

Amesema katika ziara hiyo amegundua chuo cha ufundi Arusha kina ujuzi na uwezo mkubwa wa teknolojia ikiwemo matumizi ya umeme jua kuendeshea mitambo hivyo wataona namna ya kufanya ushirikiano na chuo hicho Ili kutoa msaada kwa madereva visiwani humo.

Aidha amesema amefurahishwa na ushirikiano unaoendelea kati ya chuo cha ufundi Arusha (ATC), na kampuni ya usafirishaji ya Abnan Transport and Logistic Ltd ambapo chuo hicho kinafundisha walimu wa madereva kupitia kampuni hiyo.

“ Zanzibar tumekuwa na ongezeko la ajali za barabarani ambazo zimekuwa zikisababisha vifo na ulemavu kwa watu wengi, tunaamini ushirikiano huu unaoendelea na ule ambao tutaufanya hapo baadae utasaidia kuepusha ajali,” amesema.

Wakati huo huo, Naibu Waziri Badria amesema Serikali visiwani humo imeanza mchakato wa kuondoa matumizi ya magari ya mafuta ndani ya Serikali yake na kuanza kutumia magari ya umeme.

Amesema Serikali ya Zanzibar imeanza kubadilisha mfumo wa injinia za magari yake na kutumia umeme, na kwamba mfumo huo umeanzia kwenye magari ya umma ya usafirishaji na baadae wataendelea kwa magari ndani ya Serikali.

“ Chini ya Rais Dkt Hussein Alli Mwinyi, tumeanza kutumia magari ya umeme hasa kwa magari ya usafiri wa umma, na tutaendelea hadi kwenye magari ndani ya Serikali, naamini tutawatumia sana chuo hiki,” amesema.

Mkuu wa chuo cha ufundi Arusha Profesa Chacha Mussa akimpatia maelezo ya maendeleo ya  ujenzi wa karakana ya uchongaji wa vipuri vya magari na mitambo pamoja na fenicha inayojengwa Kwa mkopo wa Serikali ya Austria

Awali Mkuu wa Chuo cha ufundi Arusha, Profesa Mussa Chacha alisema chuo chake kimeingia ushirikiano na taasisi ya Abnan Transport and Logistic Limited ambapo walimu kutoka ATC wako visiwani humo wakiwafundisha walimu na madereva kozinya udereva.

Profesa Chacha amesema chuo cha ufundi ATC kimeshaanza utekelezaji wa Dira ya Taifa 2050 Kwa kuanzisha vitengo vitakavyotumiwa na wanafunzi kujifunza ujuzi mbalimbali kutokana na bunifu wanazozifanya chuoni hapo.

“ Tumeshaanza utekelezaji wa Dira ya Taifa 2050, hivi sasa tunajenga karakana ambayo itatumika kutengeneza vipuri vya magari na mitambo na hapa wanafunzi wetu ndio watakuwa wakitumia mitambo hiyo kuzalisha, pia jengo hilo litakuwa na karakana ya kutengeneza fenicha mbalimbali, tutakuwa tunatengeneza na kuuza,” amesema na kuongeza:

“ Pia tunakamilisha jengo la hospitali ambalo mbali ya kutoa huduma Kwa wagonjwa wanafunzi na wengine kutoka, nje pia wale wanafunzi wanaotengeneza bidhaa za hospital watatumia nafasi hiyo kujifunza badala ya kusubiri hadi waende field,” .







Post a Comment

Previous Post Next Post