Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linamshikilia Hosamu Hamza Juma, maarufu kwa jina la Maopena, kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya baba yake mzazi, Hamza Juma Omari (48), pamoja na baba yake mdogo, Ally Juma Omari (37), katika tukio lililotokea Mtaa wa Sindano, Mwananyamala, jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Julai 18, 2026 na Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Faustine Mafwele, mtuhumiwa alikamatwa Julai 17, 2026 majira ya saa 9:00 alasiri akiwa na kisu kilichokuwa na damu pamoja na mavazi yaliyoonekana kuwa na madoa ya damu, hali iliyozua shaka na kusababisha kuendelea kufanyiwa mahojiano.
Polisi wamesema kuwa wakati mahojiano hayo yakiendelea, Kituo cha Polisi Oysterbay kilipokea taarifa kutoka kwa wananchi usiku wa siku hiyo zikieleza kuwepo kwa damu nyingi katika nyumba moja iliyopo Mtaa wa Sindano, huku wakazi watatu wa nyumba hiyo wakionekana kutoweka.
Uchunguzi wa awali uliohusisha wataalamu wa uchunguzi wa kisayansi ulisababisha kugunduliwa kwa miili ya watu wawili ikiwa imefukiwa ndani ya shimo katika eneo la nyumba hiyo. Uchunguzi ulithibitisha kuwa miili hiyo ni ya Hamza Juma Omari na Ally Juma Omari.
Kwa mujibu wa Polisi, uchunguzi wa awali unamhusisha mtuhumiwa na tukio hilo, huku chanzo au sababu ya mauaji hayo ikiendelea kuchunguzwa.
Jeshi la Polisi limewapongeza wananchi na vyombo vingine vya ulinzi na usalama kwa ushirikiano walioutoa katika utoaji wa taarifa, likisema umechangia kwa kiasi kikubwa kufanikisha uchunguzi wa tukio hilo.
Aidha, Polisi wameeleza kuwa uchunguzi bado unaendelea na hatua zote za kisheria zitachukuliwa mara utakapokamilika.
SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254

Post a Comment