
Na Mapuli Misalaba, Shinyanga
Mwanaume mmoja mkazi wa
mtaa wa kalonga kata ya Ngokolo katika Manispaa ya Shinyanga anashikiliwa na Jeshi la Polisi akidaiwa
kuhusika na tuhuma za mauaji ya Mke wake Joyce
Masanja ambaye anasadikiwa ameuawa
kwa kuchomwa kisu.
Tukio hilo limetokea
usiku wa kuamkia leo Jumamosi Januari 14,2023 ambapo mwili wa mwanamke huyo umekutwa
ukiwa umetelekezwa jirani na msikiti wa Binti haji uliopo Mtaa
wa Kalonga kata ya Ngokolo.
Misalaba Blog imefika
katika eneo la tukio na kuzungumza na wakazi wa mtaa wa kalonga jina maarufu Mshikamano ambao wameeleza kuwa
tukio hilo limetokea majira ya saa sita usiku ambapo baadhi yao wamesikia sauti
ya marehemu huyo akikimbizwa na watu wawili huku akipiga kelele.
Majirani wamesema baada ya kusikia kelele hizo kwa muda
mfupi umeme ulikatika na kwamba hawakusikia tena kelele ndiyo asubuhi walimkuta
Joyce Masanja amefariki Dunia pembezoni mwa barabara jirani na msikiti wa Binti
haji.
Baadhi ya wananchi waliofika
kwenye tukio hilo wameeleza kuwa wamekuta marehemu huyo amefariki Dunia huku
akiwa amechomwa kisu sehemu mbalimbali za mwili wake ikiwepo sehemu ya shingo,
kwenye ubavu pamoja na sehemu ya mapaja yake.
Wameeleza kuwa
wamesikitishwa na tukio hilo ambapo wameilalamikia serikali ya mtaa huo kuwa
wanatoa mchango wa fedha kila mwezi kwa ajili ya ulinzi shirikishi na kwamba
ulinzi huo haufanyiki ipasavyo huku wakiliomba jeshi la polisi kufanya
uchunguzi ili kubaini chanzo cha mauaji ya Mwanamke huyo Joyce Masanja.
Kwa upande wake Mwenyekiti
wa Mtaa wa Kalonga Bwana Victor Ochieng
ameeleza kuwa amepokea taarifa za tukio hilo majira ya saa moja asubuhi
ambapo alichukua hatua za kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi,ambapo pia ametoa
rai kwa jamii kuepuka tabia ya kujichukulia sheria mkononi
Kamanda wa Jeshi la
Polisi Mkoa wa Shinyanga Kamishina Msaidizi wa polisi Janeth Magomi
amethibitisha kutokea kwa tukio hilo ambapo ameeleza taarifa za awali
zinaonyesha chanzo ni wivu wa kimapenzi baina ya Mume na Mke,na kwamba jeshi
hilo linamshikilia mwanaume huyo kwa ajili ya uchunguzi


Post a Comment