Na Fabius Clavery Misalaba Media-Kagera.Shirika la KADERES limeeleza dhamira yake ya kuendelea kusaidia wananchi wa Mkoa wa Kagera kuinuka kiuchumi kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo waliyowekeza mkoani humo.Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa KADERES, Lenard Kachebonaho, wakati akizungumza na vijana wa Mkoa wa Kagera Desemba 19, 2025, katika Kongamano la Uwekezaji lililofanyika mkoani humo kama sehemu ya Tamasha la Ijuka Omuka Akizungumza katika kongamano hilo, Kachebonaho amesema KADERES imekuwa ikiwekeza katika kuwawezesha wananchi kupitia utoaji wa elimu ya kilimo cha kibiashara pamoja na ufugaji wa nyuki, kwa kuwawezesha miche hasa wakulima wa zao la kahawa,Ufugaji wa Ng'ombe pamoja na mizinga kwa ajili ya ufugaji nyuki,ameainisha kuwa ufugaji huo huchangia kwa kiasi kikubwa kuongeza uzalishaji wa mazao kupitia mchakato wa uchavushaji. “Tunataka watoto wetu waanze kujifunza kilimo wakiwa shuleni. Zamani mwanafunzi alipokosea aliambiwa akaende kulima, hali iliyofanya kilimo kuonekana kama adhabu. Lakini ukweli ni kwamba fedha ipo shambani,” amesema Kachebonaho.Aidha, amewahimiza Watanzania, hususan wanaoishi maeneo ya pembezoni, kuacha mtazamo wa uwekezaji wa muda mfupi na badala yake kujenga misingi ya utajiri wa kudumu unaoweza kuendelea hata baada ya mmiliki kufariki. “Unakuta mtu anakuwa na biashara, lakini akifariki leo, kesho wanagawana mali na biashara inakufa. Lakini kuna watu huandaa mazingira mazuri kiasi kwamba familia inaendelea na biashara hata baada ya kifo chake, na hivyo utajiri huo kuendelea vizazi hadi vizazi. Huo ndio uwekezaji tunaotaka wananchi wauanze,” amesisitiza.Katika hatua nyingine, Kachebonaho amekemea tabia ya baadhi ya watu kuhalalisha umasikini kwa kuuita ustaarabu, huku akisisitiza umuhimu wa kuwa na maono ya kufanikiwa kiuchumi. “Mimi binafsi nilikuwa nachukia umasikini. Bahati mbaya kwa sasa kuna mwelekeo unaoendelea wa kuubariki umasikini na kuuita ustaarabu. Mtu akifanya kazi kwa bidii na kupata fedha, wapo wanaodai ni mambo ya ajabu. Lazima tubadilike na kuanza kuthamini juhudi na mafanikio ya kiuchumi,” amesema Kachebonaho.Shirika la KADERES linaendelea kushirikiana na Serikali ili kuhakikisha wananchi wa Mkoa wa Kagera wanapata maarifa, mitaji na fursa zitakazowawezesha kujenga uchumi imara na endelevu.

🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254



Post a Comment